Michezo

Liverpool wadhalilisha Palace kwa kichapo cha 7-0 ligini

December 19th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL waliweka wazi azma ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu kwa kudhalilisha Crystal Palace 7-0 mnamo Disemba 19, 2020.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Liverpool kufunga jumla ya mabao saba tangu waipepete Derby County mnamo 1991.

Ushindi huo ulitosha kusaulisha mashabiki wa Liverpool kichapo cha 7-2 ambacho kikosi chao kilipokezwa na Aston Villa kwenye EPL ugenini mnamo Oktoba 2020.

Liverpool walishambulia sana wenyeji wao baada ya kila dakika na wakasajili ushindi wa kwanza wa ligi ugenini tangu Septemba 2020.

Siku mbili baada ya kutawazwa Kocha Bora wa Mwaka 2020 katika tuzo zilizotolewa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), kocha Jurgen Klopp alimpa chipukizi Takumi Minamino fursa ya kuanza mechi katika kikosi cha kwanza na kumweka benchi fowadi Mohamed Salah.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa benchi ya klabu za EPL kuungwa na wachezaji tisa wa akiba.

Minamino aliwafungulia Liverpool ukurasa wa mabao katika dakika ya tatu. Bao hilo lilikuwa la kwanza kwa nyota huyo kufunga katika EPL baada ya miezi 12.

Sadio Mane na Roberto Firmino walifunga mabao mengine ya Liverpool katika kipindi cha kwanza. Hata hivyo, Mane alionekana kukerwa na hatua ya kuondolewa kwake uwanjani katika kipindi cha kwanza na nafasi yake kutwaliwa na Salah katika dakika ya 57.

Straika wa Liverpool Sadio Mane asherehekea baada ya kufunga bao la pili Liverpool ilikaribishwa na Crystal Palace uwanjani Selhurst Park, London, Desemba 19, 2020. Wenyeji walipoteza mchezo Liverpool ikifunga 7-0. Picha/ AFP

Henderson alipachika wavuni goli la nne la Liverpool kabla ya Firmino kupachika wavuni la tano. Salah alicheka na nyavu za Palace kwa mara nyingine katika dakika za 81 na 84 na kuzamisha kabisa chombo cha wenyeji wao.

Mchuano huo ulimpa kocha Klopp fursa ya kumchezesha kiungo Alex Oxlade-Chamberlain kwa mara ya kwanza tangu apate jeraha dhidi ya Newcastle United mnamo Julai.

Ushindi kwa Liverpool uliwawezesha kufungua mwanya wa alama sita kileleni mwa jedwali la EPL.