Michezo

Liverpool wafalme wa hela nchini Uingereza

June 8th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

LIVERPOOL imevuna matunda ya kutwaa taji la Klabu Bingwa Ulaya kwa kuibuka wafalme wa fedha kwenye orodha ya klabu zilizokuwa na mapato makubwa nchini Uingereza kutokana na upeperushaji wa mechi zao kwenye runinga.

Vijana wa Jurgen Klopp walivuna Sh12.6 bilioni kwa kuibuka namba wani barani Ulaya.

Ukiongeza mapato yao ya Sh19.6 bilioni kutoka Ligi Kuu ya Uingereza, ambayo walimaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Manchester City, walipata jumla ya mapato ya Sh32.3 bilioni, mara ya kwanza kabisa klabu yoyote imepata zaidi ya nusu bilioni ya pauni kutokana fedha za runinga katika msimu mmoja.

Hesabu hizo za fedha zilizofanywa na wataalamu wa masuala ya kifedha Swiss Ramble, zimeshuhudia Tottenham Hotspur, ambayo ilikubali kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Liverpool katika fainali ya Klabu Bingwa mnamo Juni 1 jijini Madrid nchini Ushiapnia, ikishikilia nafasi ya pili.

Spurs, ambayo ilimaliza ya nne kwenye Ligi Kuu, ilijizolea jumla ya Sh30.3 bilioni, Sh11.5 bilioni kutokana na juhudi zao za kufika fainali ya Klabu Bingwa. Vijana wa Mauricio Pochettino wanatumia Sh3.2 bilioni kila mwaka kulipa deni la Sh129 bilioni walizokopa kuongeza uwanja wao jijini London.

City, ambayo ilibanduliwa nje ya Klabu Bingwa na Spurs katika robo-fainali, inashikilia nafasi ya tatu kwa kuzoa jumla ya Sh30.08 bilioni.

Licha ya kuaga Klabu Bingwa katika robo-fainali na pia kufungiwa nje ya mduara wa timu nne za kwanza kwenye Ligi Kuu, United bado ilivuna pakubwa, jumla ya Sh29 bilioni, karibu Sh5.1 bilioni kuliko msimu 2017-2018.

Mabingwa wa Ligi ya Uropa, Chelsea, waliimarisha mapato yao hadi jumla ya Sh23.8 bilioni.

Hata hivyo, Chelsea, ambayo inafunga mduara wa tano-bora kwenye orodha ya timu zilizokuwa na mapato ya juu nchini Uingereza kwa sababu ya mechi zao kupeperushwa kwenye runinga, ilishuhudia upungufu wa mapato kwa karibu Sh1.9 bilioni.

Ilifika raundi ya 16-bora kwenye Klabu Bingwa mwaka 2018.

Kwa kurejea katika Klabu Bingwa, Chelsea itavuna Sh6.4 bilioni bila ya kupiga mpira.

United itakuwa katika orodha ya timu zitakazopoteza pakubwa msimu 2019-2020 kwa sababu zawadi kubwa itapata katika mashindano ya Bara Ulaya msimu ujao ni Sh5.1 bilioni ikishinda Ligi ya Uropa.

Arsenal, ambayo ilihitaji kucharaza Chelsea nchini Azerbaijan kujikatia tiketi ya kurejea kwenye Klabu Bingwa, imehisi pigo la kukosa mashindano hayo ya daraja ya juu kwa misimu miwili. Imeambulia Sh22.4 bilioni kwa juhudi zake ligini na katika Ligi ya Uropa.

Mwanya waongezeka

Hata hivyo, mwanya kati ya Arsenal na Spurs uliongezeka kutoka Sh3 bilioni mwaka 2018 hadi Sh7.8 bilioni mwaka 2019, huku Spurs ikitarajiwa kuuongeza hata zaidi msimu 2019-2020 baada ya kumaliza Ligi Kuu katika nafasi ya nne.

Mapato yanaonyesha kuwa Arsenal ilipata Sh9.8 bilioni chini ya Liverpool, tofauti kubwa kati ya timu ambazo zilikuwa nafasi tatu pekee kutoka kwa nyingine kwenye Ligi Kuu.

Hesabu hizo si nzuri kwa Arsenal, ingawa kwa Wolves, itakuwa nafasi nzuri ya kuimarisha hali yake ya kifedha baada ya kuingia Ligi ya Uropa.

Everton, ambayo ni nambari saba kwenye ligi ya fedha nchini Uingereza na haitashiriki mashindano ya Bara Ulaya, ilizoa Sh16.5 bilioni.

Wolves, ambayo ilikuwa Sh180.5 milioni nyuma, sasa inatarajiwa kuzoa Sh2.3 bilioni ama zaidi ikipita mechi za mchujo na zile za makundi kwenye Ligi ya Uropa.