Liverpool wafungua kampeni za EPL 2022-23 kwa sare ya 2-2 dhidi ya Fulham

Liverpool wafungua kampeni za EPL 2022-23 kwa sare ya 2-2 dhidi ya Fulham

Na MASHIRIKA

DARWIN Nunez alitokea benchi na kufunga bao kabla ya kuchangua jingine katika gozi la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) lililowashuhudia wakitoka nyuma mara mbili na kulazimishia Fulham sare ya 2-2 mnamo Agosti 6, 2022 ugani Craven Cottage.

Liverpool waliopigwa kumbo na Manchester City katika kampeni za EPL katika dakika za mwisho za kampeni za msimu uliopita wa 2021-22, walijipata chini baada ya Aleksandar Mitrovic aliyepokea krosi ya Kenny Tete kumzidi ujanja Trent Alexander-Arnold.

Luis Diaz wa Liverpool alishuhudia bao lake likifutiliwa mbali baada ya teknolojia ya VAR kubaini kwamba alikuw ameotea.

Nunez aliyekuwa akicheza kwa mara ya kwanza katika EPL, aliwarejesha Liverpool mchezoni katika dakika ya 64 kabla ya Mitrovic aliyechezewa visivyo na beki Virgil van Dijk kufunga bao la pili la Fulham kupitia mkwaju wa penalti.

Liverpool walisawazishiwa na Mohamed Salah baada ya kumegewa pasi na Nunez aliyesajiliwa na kutoka Benfica ya Ureno kwa Sh9.2 bilioni.

Mara ya mwisho kwa Fulham kushinda mechi katika EPL ni mnamo Machi 7, 2021 dhidi ya Liverpool. Wakati huo, ushindi huo haukutosha kuwaepushia shoka lililowateremsha ngazi katika EPL.

Fulham walilazimika kusubiri hadi mechi ya tano kujizolea alama kwenye EPL mara ya mwisho walipoanza kampeni za EPL mnamo 2020-21.

Hii ilikuwa mara ya nne mfululizo kwa Liverpool kufungua kampeni zao za EPL dhidi ya kikosi kilichopandishwa ngazi kutoka Ligi ya Daraja ya Kwanza nchini Uingereza (Championship).

Chini ya kocha Jurgen Klopp, kikosi hicho kiliambulia nafasi ya pili kwenye EPL mnamo 2021-22 kwa alama 92, moja pekee nyuma ya Man-City. Masogora hao wa kocha Jurgen Klopp walikosa huduma za wachezaji Curtis Jones, Diogo Jota, Konstantinos Tsimikas, Naby Keita, Alex Oxlade-Chamberlain na Ibrahima Konate.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Ruto: Hata Uhuru atafurahia enzi ya utawala wangu endapo...

MKU yakabidhiwa cheti cha ubora kutoka KEBS

T L