Michezo

Liverpool wakataza Coutinho kurejea Anfield

April 28th, 2020 2 min read

CHRIS ADUNGO na MASHIRIKA

LIVERPOOL wamemweleza Philippe Coutinho kwamba hawapo tayari kuwania upya huduma zake mwishoni mwa msimu huu baada ya ajenti wa kiungo huyo, Kia Joorabchian kuulizia uwezekano wa kurejea kwa mteja wake ugani Anfield.

Coutinho ametatizika sana kufufua makali aliyokuwa akijivunia zamani uwanjani Anfield kabla ya kuyoyomea Uhispania kuvalia jezi za Barcelona mnamo Januari 2018.

Barcelona walimshawishi Coutinho, 27, kuagana na Liverpool kwa kima cha Sh14 bilioni japo akashindwa kusadikisha mashabiki wa miamba hao kwamba alistahili kununuliwa kwa kiwango hicho cha fedha.

Kushindwa kwake kutamba ugani Camp Nou ni kiini cha Barcelona kumtuma kwa mkopo wa mwaka mmoja kambini mwa Bayern Munich mwanzoni mwa msimu huu.

Japo ilitarajiwa kwamba Bayern wangalikuwa wepesi wa kumpokeza mkataba wa kudumu, mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) hawajaonyesha ari ya kuziwania huduma za nyota huyo mzawa wa Brazil.

Badala yake, ameanza kuhusishwa na uwezekano mkubwa wa kuingia kambini mwa Leicester City ambao kwa sasa watalazimika kuwapiga kumbo Everton, Chelsea na Manchester United wanaomkeshea sogora huyo.

Kwa mujibu wa Joorabchian, kubwa zaidi katika maazimio ya Coutinho ni kurejea Uingereza kuvalia jezi za kikosi chochote cha EPL iwapo Barcelona wataamua kumtia mnadani.

Kocha Brendan Rodgers aliyemsajili Coutinho kambini mwa Liverpool yuko tayari kushawishi Leicester kufungulia mifereji yao ya fedha na kumsajili kiungo huyo ambaye pia ni kivutio kikubwa cha kocha Carlo Ancelotti wa Everton.

Ingawa hivyo, Barcelona wako tayari kumdumisha Coutinho kambini mwa Bayern kwa msimu mwingine mmoja wa mkopo iwapo hakuna kikosi kitakachomuda bei yake mpya ya Sh10 bilioni.

Hadi alipobanduka ugani Anfield, Coutinho alikuwa ametawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka kambini mwa Liverpool mara mbili na alikuwa amepachika wavuni zaidi ya mabao 50 katika kipindi kizima cha misimu mitano.

Ujio wa kocha Jurgen Klopp uwanjani Anfield ulimkosesha Coutinho nafasi katika kikosi cha kwanza cha Liverpool. Hii ni baada ya mfumo mpya ulioletwa na Klopp kutowiana na mtindo wa kucheza kwa Coutinho ambaye alipachika wavuni mabao 21 kutokana na mechi 76 ugani Camp Nou.