Liverpool wakomoa Arsenal na kupiga breki rekodi ya kutoshindwa kwao katika mechi 10

Liverpool wakomoa Arsenal na kupiga breki rekodi ya kutoshindwa kwao katika mechi 10

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL walikomesha rekodi nzuri ya kutoshindwa kwa Arsenal katika mechi 10 mfululizo kwenye mashindano yote kwa kuwapepeta 4-0 ugani Anfield.

Sadio Mane aliwafungulia Liverpool ukurasa wa mabao kupitia frikiki ya Trent Alexander-Arnold katika dakika ya 39. Diogo Jota alichuma nafuu kutokana na masihara ya beki Nuno Tavares na kupachika wavuni bao la pili kabla ya Mohamed Salah kufunga la tatu kupitia krosi ya Mane.

Beki Alexander-Arnold alichangia bao la nne ambalo Liverpool walifungiwa na Takumi Minamino aliyecheka na nyavu za wageni wao sekunde 48 pekee baada ya kutokea benchi.

Ushindi ulipaisha Liverpool hadi nafasi ya pili kwenye jedwali la EPL kwa alama 25 huku Arsenal wakisalia katika nafasi ya tano kwa pointi 20.

Liverpool wangalifunga mabao zaidi kupitia Salah, Alexander-Arnold na Thiago Alcantara ila wakazidiwa ujanja na kipa Aaron Ramsdale.

Majaribio ya Pierre-Emerick Aubameyang na Bukayo Saka langoni mwa Liverpool yalizimwa kirahisi na kipa Alisson Becker aliyeshirikiana vilivyo na mabeki Virgil van Dijk na Joel Matip.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Kocha Xavi ashinda mechi yake ya kwanza akidhibiti mikoba...

Majibizano hatari kwa Ruto Mlimani

T L