Michezo

Liverpool wakomoa Brentford na kukatalia pale juu mezani

February 17th, 2024 1 min read

NA MASHIRIKA

LIVERPOOL waliendelea kudhibiti usukani wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na kujiweka pazuri kutawazwa mabingwa wa kipute hicho msimu huu baada ya kutandika Brentford 4-1 uwanjani Brentford Community Stadium.

Darwin Nunez aliwafungulia Liverpool ukurasa wa mabao kunako dakika ya 35 kabla ya magoli mengine kufumwa wavuni katika kipindi cha pili kupitia kwa Alexis Mac Allister, Mohamed Salah na Cody Gakpo.

Bao la Salah lilikuwa lake la kwanza mwaka huu akivalia jezi za Liverpool. Nyota huyo raia wa Misri alikuwa akiwajibikia Liverpool kwa mara ya kwanza tangu apate jeraha la paja mwezi uliopita akicheza dhidi ya Ghana kwenye fainali za Kombe la Afrika (AFCON) nchini Ivory Coast.

Chini ya kocha Jurgen Klopp, Liverpool sasa wanajivunia alama 57 kutokana na mechi 25 na pengo la pointi tano linatamalaki kati yao na nambari tatu Arsenal walio na mchuano mmoja zaidi wa akiba. Hata hivyo, raha ya ushindi wa Liverpool iliyeyushwa na majeraha yaliyomlazimisha Klopp kuwaondoa uwanjani wanasoka Curtis Jones, Diogo Jota na Nunez katika kipindi cha kwanza.

Brentford wanajivunia alama 25 kutokana na michuano 24. Walifutiwa machozi na Ivan Toney kunako dakika ya 75.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO