Michezo

LIVERPOOL WALA RUNGU! Watford yakatiza matumaini ya Reds kumaliza msimu wa EPL bila kupoteza mechi yoyote

March 2nd, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

MERSEYSIDE, Uingereza

KOCHA Jurgen Klopp amewataka Liverpool kujinyanyua haraka katika mechi zijazo, baada ya Watford kukatiza ghafla matumaini yao ya kumaliza msimu huu bila kupoteza gozi lolote kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Kichapo cha 3-0 walichopokezwa Liverpoool uwanjani Vicarage Road siku ya Jumamosi, kiliwatoa Watford katika mduara hatari wa kutemwa nje ya EPL.

Nyota Ismaila Sarr kutoka Senegal ndiye alikuwa staa wa mechi hiyo alipowafungia Watford mabao mawili huku nahodha Troy Deeney akitia ndani la tatu.

Lakini kichapo hicho pia kiliwaletea mashabiki wa Arsenal, almaarufu Gunners, raha tele kwani kilidumisha rekodi yao ya 2003-04 ambapo Gunners walishinda EPL bila kushindwa katika mechi yoyote ya ligi.

Hadi waliposhuka dimbani Jumamosi, Liverpool walikuwa wamesalia na ushindi mara tano pekee ili kufikia rekodi ya Arsenal. Gunners wanajivunia kupiga idadi kubwa zaidi ya mechi (49) bila kupoteza katika historia ya soka ya Uingereza.

Watford ndiyo timu ya kwanza kuwapiga Liverpool katika EPL tangu Manchester City wawabwage miamba hao Januari 2019. Kichapo hicho ndicho kinono zaidi ambacho timu inayoongoza jedwali la EPL imewahi kupokezwa, tangu Novemba 2015 ambapo Liverpool walipepeta Man-City magoli 4-1.

Aidha, huo ndio ushindi mnono zaidi kuwahi kusajiliwa na timu iliyo hatarini kutemwa nje ya EPL dhidi ya klabu inayoselelea uongozini. Mara ya mwisho kwa hali hii kutokea ni wakati Leicester City ilikomoa Manchester United mabao 3-0 mnamo Novemba 23, 1985.

Ilikuwa mara ya kwanza tangu Machi 2019 kwa Liverpool kushindwa kufunga bao katika EPL, tukio lililokomesha rekodi ya awali iliyowashuhudia wakitikisa nyavu za wapinzani katika michuano 36 mfululizo.

Kufikia sasa, Liverpool wamefungwa idadi kubwa zaidi ya mabao katika michuano miwili mfululizo (magoli matano) tangu Disemba 2016. Kabla ya kuvaana na Watford, walikuwa wamewapiga West Ham United 3-2 uwanjani Anfield katika mechi ya ligi, kisha kupepetwa 1-0 na Atletico Madrid katika mechi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) nchini Uhispania.

Kufikia Jumamosi, Liverpool walikuwa wamejizolea ushindi katika msururu wa michuano 18 ya EPL, rekodi sawa na Man-City msimu uliopita.

Ufanisi mwingine ugani Vicarage Road ungewafanya kuwa timu yenye rekodi ndefu zaidi ya ushindi katika historia ya kipute hicho.

Ingawa hivyo, Klopp ameshikilia kwamba kubwa zaidi katika maazimio yao msimu huu halikuwa kuandikisha rekodi zozote, bali kutia kapuni mataji muhimu.

Chini ya Klopp, Liverpool wako pua na mdomo kujitwalia ubingwa wa EPL kwa mara ya kwanza katika miaka 30, wakiwa alama 22 mbele ya nambari mbili Man-City. Tayari wanajivunia mataji ya Super Cup, Kombe la Klabu Bingwa Duniani (Club World Cup) na bado wanatetea taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Isitoshe, bado wanafukuzia ufalme wa Kombe la FA na taji la (UEFA) ambalo wameapa kulitetea kwa mafanikio.

Zikisalia mechi 10 pekee kabla ya kivumbi cha EPL kutamatika rasmi, Liverpool wanashikilia uongozi kwa alama 79 huku pengo la pointi 22 likitamalaki kati yao na mabingwa watetezi Man-City, ambao ni wa pili.

Liverpool kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Chelsea katika raundi ya tano ya FA siku ya Jumatano, kabla ya kuwaalika Bournemouth ligini mwisho wa wiki hii.

Kwa upande wao, Watford wameratibiwa kuchuana na Crystal Palace, Leicester na Burnley kwa usanjari huo.