Michezo

Liverpool wapiga Ajax kwenye UEFA licha ya visa vingi vya majeraha

October 22nd, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

MABINGWA wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Liverpool walisajili ushindi katika mchuano wao wa kwanza wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu wa 2019-20 kupitia bao la Nicolas Tagliafico aliyejifunga kwa upande wa Ajax nchini Uholanzi.

Kocha Jurgen Klopp aliongoza kikosi chake kunogesha kipute hicho bila maarifa ya baadhi ya wanasoka tegemeo, akiwemo beki Virgil van Dijk.

Tagliafico alishindwa kudhibiti kombora ambalo fowadi Sadio Mane alielekeza langoni mwao kunako dakika ya 35.

Bao hilo lilijazwa wavuni muda mfupi baada ya kipa Adrian Miguel wa Liverpool kumnyima Quincy Promes fursa nzuri ya kuwaweka Ajax kifua mbele.

Liverpool ambao pia watavaana na Atalanta ya Italia na Midtjylland ya Denmark kwenye Kundi D, walikuwa wakirejea kunogesha soka ya UEFA wakishikilia ubingwa wa EPL kwa mara ya kwanza tangu 1984-85.

Mbali na Van Dijk, Liverpool walijibwaga ugani kwa minajili ya mechi hiyo bila ya kujivunia pia maarifa ya wanasoka Joel Matip, Thiago Alcantara na kipa Alisson Becker ambaye nafasi yake ilitwaliwa na Adrian.

Kutokuwepo kwa Matip na Van Dijk kulimsaza Klopp katika ulazima wa kutegemea huduma za beki Joe Gomez aliyeshirikiana vilivyo na Fabinho.

Liverpool ambao ni mabingwa mara sita wa UEFA, walishuka dimbani wakilenga kusajili ushindi wa kwanza wa mwezi Oktoba katika jaribio la nne, baada ya Everton kuwalazimishia sare ya 2-2 kwenye Debi ya Merseyside mnamo Oktoba 17, 2020 ugani Goodison Park.

Awali, masogora hao wa Klopp walikuwa wamebanduliwa na Arsenal nje ya kivumbi cha Carabao Cup hatua ya 16-bora, kwa kichapo cha 5-4 kupitia mikwaju ya penalti mnamo Oktoba 1 kabla ya Aston Villa kuwadhalilisha kwa magoli 7-2 ligini mnamo Oktoba 4.

Kizungumkuti zaidi kwa Liverpool kwa sasa ni kwamba huenda wakamkosa Van Dijk katika kampeni zote zilizosalia muhula huu kufuatia thibitisho kwamba Mholanzi huyo atafanyiwa upasuaji wa goti, baada ya kuchezewa visivyo na kipa Jordan Pickford wa Everton.

Liverpool kwa sasa hawajapoteza mechi yoyote kati ya saba zilizopita dhidi ya kikosi cha Ligi Kuu ya Uholanzi ugenini. Wapambe hao wamesajili ushindi mara nne na kuambulia sare mara tatu.

Liverpool wanarejea ugani kwa kampeni za EPL mnamo Oktoba 24 watakapowaalika Sheffield United uwanjani Anfield kabla ya kuwa wenyeji wa Midtjylland kwenye UEFA mnamo Oktoba 27.