Michezo

Liverpool wapiga Ajax na kusonga mbele UEFA huku chipukizi Curtis Jones akiweka historia

December 2nd, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

CHIPUKIZI Curtis Jones wa Liverpool alifunga bao lake la kwanza katika kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) baada ya kuchuma nafuu kutokana na kosa la kipa Andre Onana wa Ajax mnamo Disemba 1, 2020 uwanjani Anfield, Uingereza.

Ushindi huo uliosajiliwa na Liverpool uliwasaidia kufuzu kwa hatua ya 16-bora ya UEFA kutoka Kundi D wakiwa kileleni.

Onana alichelewa kufikia mpira uliolekezwa langoni mwake na Neco Williams na kusuasua kwake kumpa Jones, 19, fursa ya kucheka na nyavu katika dakika ya 58.

Kipa Caoimhin Kelleher aliyewajibishwa na Liverpool katika nafasi ya mlinda-lango chaguo la kwanza, Alisson Becker pia alichangia pakubwa ushindi wa Liverpool baada ya kufanya kazi ya ziada ya kupangua fataki alizoelekezewa na fowadi Klaas-Jan Huntelaar aliyeingia uwanjani katika kipindi cha pili.

Kiungo wa zamani wa Everton, Davy Klaassen naye alipoteza nafasi nyingi za wazi huku David Neres akishuhudia kombora lake likibusu mwamba wa lango la Liverpool sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchuano kupulizwa.

Jones naye alishuhudia fataki yake ikigonga mhimili wa lango la Ajax dakika nne kabla ya kucheka na nyavu za wageni wao. Liverpool ambao kwa sasa watacheza na Midtjylland ya Denmark katika mchuano wao wa mwisho kundini mnamo Disemba 9, wanaungana na Manchester City na Chelsea ambao ni wawakilishi wengine wa soka ya Uingereza ambao tayari wamefuzu kwa hatua ya 16-bora ya UEFA msimu huu.

Liverpool walishuka dimbani wakitawaliwa na kiu ya kusajili ushindi ili kuepuka presha ambayo vinginevyo ingewakosesha dira baada ya Atalanta ya Italia kuwaduwaza kwa kichapo cha 2-0 katika mechi nyingine ya Kundi D uwanjani Anfield wiki moja iliyopita.

Baada ya Atalanta kulazimishiwa sare ya 1-1 na Midtjylland nchini Denmark, Liverpool kwa sasa wanajivunia alama 12, nne zaidi kuliko nambari mbili Atalanta kwenye Kundi D.

Huku Liverpool wakitumia mchuano dhidi ya Ajax kumkaribisha kikosi nahodha Jordan Henderson aliyekuwa akicheza kwa mara ya kwanza tangu Novemba 8 kwa sababu ya jeraha, Liverpool walifichua kwamba kipa Alisson huenda sasa akasalia mkekani kwa kipindi kirefu.

Jeraha la Alisson ambaye sasa atakosa mechi mbili zijazo za Liverpool dhidi ya Wolves kwenye EPL na Midtjylland kwenye UEFA, linamaanisha kwamba kocha Jurgen Klopp atakosa maarifa ya wanasoka tisa wa kikosi cha kwanza wakiwemo Naby Keita, Trent Alexander-Arnold, Virgil van Dijk, Joe Gomez, Xherdan Shaqiri, James Milner, Thiago Alcantara na Alex Oxlade-Chamberlain.

Maamuzi ya Klopp kumchezesha kipa Kelleher dhidi ya Ajax badala ya Adrian ambaye amekuwa siku zote akichukua nafasi ya Alisson, yanaibua maswali mengi kuhusu mustakabali wa Adrian uwanjani Anfield.

Adrian aliyesajiliwa mwanzoni mwa msimu wa 2019-20, anajivunia kucheza zaidi ya mechi 200 zilizopita akivalia jezi za Real Betis, West Ham United na Liverpool.

Jones (miaka 19 na siku 306) ndiye mchezaji wa tatu mwenye umri mchanga zaidi kuwahi kufungia Liverpool kwenye UEFA baada ya David N’Gog mnamo 2008 (miaka 19 na siku 252 dhidi ya PSV Eindhoven) na Trent Alexander-Arnold mnamo 2017 (miaka 19 na siku 10 dhidi ya Maribor).