Liverpool warukia nafasi ya pili jedwalini baada ya kupiga Brentford katika EPL

Liverpool warukia nafasi ya pili jedwalini baada ya kupiga Brentford katika EPL

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL walipaa hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kupepeta limbukeni Brentford 3-0 ugani Anfield.

Fabinho aliwafungulia Liverpool ukurasa wa mabao mwishoni mwa kipindi cha kwanza kabla ya Alex Oxlade-Chamberlain na Takumi Minamino kufunga mengine kupitia mchango wa Andy Robertson.

Chini ya kocha Jurgen Klopp, Liverpool kwa sasa wanajivunia alama 45 huku pengo la pointi 11 likitamalaki kati yao na mabingwa watetezi Manchester City wanaoselelea kileleni mwa jedwali. Hata hivyo, Liverpool wana mechi moja zaidi ya kutandaza ili kufikia idadi ya michuano 22 ambayo tayari imesakatwa na Man-City.

Tofauti na Man-City ambao wamepoteza alama 10 pekee msimu huu, Liverpool wameshinda michuano 13, kuambulia sare mara sita na kupigwa mara mbili kutokana na mechi 21 zilizopita ligini.

Ilikuwa mara ya kwanza tangu Mei 2017 kwa Liverpool kusuka kikosi cha EPL kilichokosa huduma za ama Mohamed Salah au Sadio Mane ambao sasa wanasakatia Misri na Senegal mtawalia kwenye fainali za Kombe la Afrika (AFCON) zinazoendelea nchini Cameroon.

Liverpool walishuka dimbani kwa ajili ya mechi hiyo siku tatu baada ya Arsenal kuwalazimishia sare tasa kwenye mchuano wa mkondo wa kwanza wa nusu-fainali za Carabao Cup ugani Anfield.

Brentford waliolazimishia Liverpool sare ya 3-3 katika mkondo wa kwanza mnamo Septemba 2021, sasa wanakamata nafasi ya 14 kwa alama 23 sawa na Aston Villa. Hii ni mara yao ya kwanza katika kipindi cha miaka 74 kwa Brentford kunogesha kipute cha EPL.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

AFCON: Gambia na Mali pazuri kuingia hatua ya 16-bora baada...

Ajabu ya mjane kupoteza mamilioni kwa kupenda jini

T L