Michezo

Liverpool wasajili kipa Marcelo Pitaluga kutoka Fluminense nchini Brazil

October 9th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Liverpool, wamekamilisha usajili wa kipa Marcelo Pitaluga kutoka Fluminense.

Marcelo alikuwa sehemu ya kikosi kilichoshindia Brazil ubingwa wa Kombe la Dunia kwa chipukizi wa U-17 mnamo Novemba 2020.

Ushawishi wake kambini mwa Brazil wakati huo ulimpa fursa ya kuwajibishwa katika kikosi cha kwanza cha Fluminense kwa ushirikiano na Muriel ambaye ni kaka mdogo wa kipa chaguo la kwanza la Liverpool, Alisson Becker.

“Nilimuona kwa mara ya kwanza wakati wa fainali za Kombe la Dunia. Tumetalii soko zima la uhamisho wa wachezaji na tukapata ndiye wa pekee aliye na uwezo wa kusaidiana na Adrian Sam Miguel langoni mwetu tunapozidi kumsubiri Alisson arejee baada ya kupona jeraha,” akasema mkuu wa makipa ugani Anfield, John Achterberg.

Kwa mujibu wa kocha Jurgen Klopp wa Liverpool, huenda Alisson akasalia nje kwa zaidi ya majuma manne baada ya kurejelewa kwa kivumbi cha EPL kitakachopisha mechi za kimataifa mwishoni mwa wiki hii.

Ina maana kwamba Liverpool wataendelea kutegemea huduma za kipa Adrian San Miguel aliyejiunga nao msimu uliopita kutoka West Ham United.

Baada ya kupepetana na viongozi wa jedwali Everton wikendi hii, Liverpool watawaendea Ajax katika Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kabla ya kurejelea kampeni za EPL dhidi ya Sheffield United mnamo Oktoba 24, 2020.