Michezo

Liverpool watembea kwa upweke jijini Madrid

February 20th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

MADRID, Uhispania

WALIPOTEREMKA uwanjani Wanda Metropolitano jijini Madrid mnamo Jumanne usiku, Liverpool walikuwa wametunatuna kama andazi moto kwa imani ya kushinda Atletico Madrid.

Lakini kipenga cha mwisho kilipolia, vijana wa Jurgen Klopp walikuwa hoi bila pumzi baada ya kutobolewa 1-0 na Madrid, ambao vyombo vya habari vilikuwa vimebashiri wangepewa kichapo cha mbwa na wageni wao.

Bao la Saul Niguez lilitosha kuzima makeke ya mabingwa watetezi wa kombe hilo, ambao msimu huu wanatamba katika Ligi Kuu ya Uingereza wakiwa hawajapoteza mechi yoyote kufikia sasa.

Kichapo hicho kilimuuma sana Klopp, ambaye aliapa kuchapa Madrid kwenye mechi ya marudiano na kufuzu kwa robo fainali ya dimba hilo.

“Tulishindwa 1-0, lakini nina matumaini makubwa tutabadilisha matokeo haya mbele ya mashabiki wetu Anfield na kuendelea na kampeni za kutetea taji,” aliongeza.

Hata hivyo, haitakuwa kazi rahisi kwa vile watakuwa wakicheza na timu inayojivunia kocha mwenye maarifa ya kutosha katika mechi kubwa Diego Simeone, ambaye anafahamika kwa kuangusha vigogo katika mechi za awali.

Kichapo cha Madrid hakikumfurahisha kocha Klopp pamoja na beki Andy Robertson ambao wote kwa sasa wanaamini ilikuwa bahati mbaya.

Klopp aliwashutumu mashabiki wa Madrid kwa kujaribu kumshinikiza refa amuonyeshe kadi nyekundu Sadio Mane huku Robertson akiwaonya wapinzani wao wasitarajie kazi rahisi ugani Anfield.

Wakati huo huo, mashabiki wa Liverpool wamemlaumu vikali beki wao tegemeo Virgil van Dijk kwa kushindwa kumzuia Niguez kufungia Madrid bao.

Beki huyo kadhalika alilaumiwa na mzimulizi wa kituo cha beIN SPORTS, Rudd Gullit, aliyedai mbali na kosa hilo, nahodha huyo wa timu ya Uhoanzi alifanya makosa mengine.

“Huenda wanatarajia kufunga mabao mengi pale Anfield, lakini huenda mambo yakawa magumu siku hiyo,” Gullit aliongeza.