Michezo

Liverpool watoka nyuma na kurefusha mkia wa Sheffield United kwenye EPL

October 25th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Liverpool walitoka nyuma na kuwapokeza Sheffield United kichapo cha 2-1 katika mchuano uliochezewa uwanjani Anfield mnamo Oktoba 24, 2020.

Fabinho aliyeaminiwa kujaza nafasi ya beki Virgil van Dijk anayeuguza jeraha, alisababisha penalti iliyowaweka Sheffield kifua mbele kunako dakika ya 13. Penalti hiyo iliyofungwa na Sander Berge ilitokana na tukio la Fabinho kumchezea Oliver McBurnie visivyo ndani ya kijisanduku.

Licha ya Liverpool kuonekana kuzidiwa maarifa katika safu ya kati na kuwekewa presha zaidi na Sheffield, masogora hao wa kocha Jurgen Klopp walipata bao la kwanza katika dakika ya 41 baada ya Roberto Firmino kushirikiana vilivyo na Sadio Mane.

Liverpool waliingia uwanjani wakitawaliwa na kiu ya kusajili ushindi baada ya kupigwa kwenye mechi mbili zilizopita ikiwemo ile iliyowashuhudia wakipepetwa 7-2 na Aston Villa. Ushindi wa Liverpool uliwawezesha kuchupa hadi kileleni mwa jedwali la EPL kwa alama 13 sawa na watani wao wakuu wa Merseyside, Everton ambao watavaana na Southampton uwanjani St Mary’s mnamo Oktoba 24.

Bao la pili la Liverpool lilifungwa na sajili mpya Diogo Jota katika dakika ya 64 baada ya kushirikiana vilivyo na Mohamed Salah ambaye kwa pamoja na beki Trent Alexandre-Arnold, walipoteza nafasi nyingi za wazi.

Chini ya kocha Chris Wilder, Sheffield United hawajasajili ushindi wowote kutokana na mechi sita zilizopita na wanajivunia alama moja pekee sawa na limbukeni Fulham waliopigwa 2-1 na Crystal Palace uwanjani Craven Cottage mnamo Oktoba 24.

Jeraha ambalo litamweka Van Dijk mkekani kwa kipindi kirefu kijacho linamweka Klopp katika ulazima wa kutegemea Fabinho na Joe Gomez kwenye safu ya ulinzi hadi mwishoni mwa Novemba 2020 ambapo wawili hao watapigwa jeki na Joel Matip atakayekuwa amepona jeraha.

Liverpool kwa sasa wameshinda mechi nne zilizopita za EPL dhidi ya Sheffield United kwa jumla ya mabao 9-1. Mabingwa hao watetezi wa EPL wanajivunia pia rekodi ya kushinda mechi 28 za ligi kati ya 29 zilizopita uwanjani Anfield. Chini ya Klopp, Liverpool hawajapoteza pia mechi 13 zilizopita ambazo zimewashuhudia wakifungwa kwanza na wapinzani wao.

Kufikia sasa, Liverpool wamefungwa mabao 14 kutokana na mechi sita za kwanza za EPL msimu huu. Katika kampeni za muhula wa 2019-20, iliwachukua jumla ya mechi 15 kwa nyavu zao kutikiswa mara hizo.

Jota ni mchezaji wa pili baada ya Mane mnamo Septemba 2016, kufunga bao katika mechi mbili za kwanza za Liverpool uwanjani Anfield.

Liverpool kwa sasa wanajiandaa kuwaalika FC Midtjylland katika mechi yao ya pili ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Oktoba 27 uwanjani Anfield kabla ya kuvaana na West Ham United ligini mnamo Oktoba 31.

Kwa upande wao, Sheffield United watawaalika Manchester City ugani Bramall Lane mnamo Oktoba 27 kabla ya kuwaendea Chelsea uwanjani Stamford Bridge wiki moja baadaye.