Michezo

Liverpool yasisitiza itawatoa City kijasho katika EPL

March 5th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

MERSEYSIDE, UINGEREZA

KOCHA Jurgen Klopp wa Liverpool amesema anaridhishwa zaidi na hali ya sasa inayowasaza katika ulazima wa kufukuzia Manchester City kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Liverpool walipoteza udhibiti wao wa kilele cha jedwali la EPL mwishoni mwa wiki jana baada ya kuambulia sare tasa dhidi ya Everton katika gozi kali la Meseryside lililowakutanisha ugani Goodison Park.

Matokeo hayo yaliwateremsha Liverpool katika nafasi ya pili jedwalini kwa mara ya kwanza tangu Desemba 7, 2018.

Kufikia sasa, Liverpool wanajivunia alama 70, moja nyuma ya Manchester City ambao wamesisitiza wanalenga kutia kapuni mataji manne katika kampeni za msimu huu.

Baada ya kuwacharaza Chelsea na kutwaa Carabao Cup, masogora wa kocha Pep Guardiola pia wana ari ya kutia kapuni ubingwa wa Kombe la FA, ufalme wa UEFA na kutetea kwa mafanikio taji la EPL.

Tottenham waliolazimishiwa sare ya 1-1 na Arsenal katika gozi la London Kaskazini mnamo Jumamosi, wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama 61, tatu zaidi mbele ya Manchester United ambao wanafunga mduara wa nne-bora.

Chelsea ambao wana mchuano mmoja zaidi wa kutandaza wanashikilia nafasi ya sita kwa alama 56, moja kuliko Arsenal. Zimesalia mechi tisa zaidi kwa kampeni za EPL muhula huu kutamatika rasmi.

Hadi kufikia mwisho wa mwaka jana, Liverpool walikuwa wakijivunia pengo la alama saba kati yao na Manchester City ambao walipunguza zaidi pointi hizi baada ya kusajili ushindi dhidi ya wapinzani wao hao katika mchuano uliowakutanisha ugani Etihad mnamo Januari 3.

Ingawa Liverpool walisajili ushindi katika mechi mbili baadaye, vijana hao wa Klopp wamelazimishiwa sare nne katika jumla ya mechi sita zilizopita.

“Presha kwa sasa iko kwa Man-City ambao watapania kudumisha nafasi yao kileleni mwa jedwali katika takriban kila mchuano,” akasema Klopp katika mawazo yaliyoungwa na beki Andrew Robertson.

“Muhimu zaidi kwa sasa ni kumakinikia kila mchuano uliopo mbele yetu hatua kwa hatua. Presha ambayo Manchester City wamekuwa nayo katika juhudi za kutetea ubingwa wa EPL sasa itazidishwa na tukio hili la sisi kuwafukuzia kileleni,” akasema difenda huyo mzawa wa Scotland.

Liverpool walihitaji ushindi dhidi ya Everton ili kuwaruka Man-City ambao awali walikuwa wamewapepeta Bournemouth 1-0 uwanjani Dean Court.