Habari Mseto

Lo! si mabinti pekee ‘wachimba migodi’, madume pia hatari sana

July 25th, 2020 2 min read

NA MWANDISHI WETU

Tangu jadi jamii imefinyanga mawazo yetu kudhania kwamba mabinti pekee ndio walio na tabia ya kufaidika kutokana na mifuko ya wanaume; yaani kama wanavyotambulika kwa lugha isiyo rasmi – wachimba migodi.

Lakini kwa kweli nyakati hizi ni tofauti, na usawa umekumbatiwa na jinsia zote. Kuambatana na mada hii, sawa na baadhi ya mabinti wanaotumia urembo na chombo walichopachikwa mapajani kama kitega uchumi, pia kuna madume wanaofanya vivyo hivyo kwa minajili ya kunufaika kifedha.

Katika ulimwengu wa sasa, kuna madume wanaotumia utanashati wao kunasa mapenzi ya mabinti wenye mifuko mizito.Mara nyingi akina kaka hawa hushughulika sana na mwonekano wao, na muda wao mwingi wanautumia kwa kuhakikisha kwamba wanapendeza kila mara.

Wanajua kuvalia nadhifu na mavazi yao huwasitiri vyema na kuonyesha maumbo yao ya kupendeza. Nguo zao huwa za bei ghali, tena mtindo wa kisasa.

Mavazi yao kutoka kwa shati, longi, kiatu na mshipi yanaakisi gharama, na wakipita karibu nawe, hauna budi ila kusalia ukipiga chafya kwani wanapenda kujipulizia marashi yenye harufu kali.

Vichwa na ndevu zao huwa zimechengwa sawasawa kila siku ya wiki. Kucha zao hushughulikiwa angaa kila baada ya majuma mawili, na ukiwasalimu, utagundua kwamba mikono yao ni miororo hata zaidi ya makalio ya mtoto mchanga.

Mara nyingi wamejaliwa kisura na na mwonekano wao hasa unakamilishwa na maumbo yao yaliyopigwa msasa na mazoezi wanayofanya kila wakati.

Wengi wao wamejiweka katika maisha ya hali ya juu, na mara nyingi burudani zao huwa katika baa na hoteli za haiba ya juu.

Haya ni mazingira mwafaka ya kunasa mabinti wenye mifuko mizito ambao hasa husaidia kufadhili maisha yao ghali. Kwenye mitandao ya kijamii, uwepo wako unatikisa kila mara kwani hawachelewi kuchapisha picha mpya kila wakati.

Nia yao hasa huwa kuwafanya mabinti kudhani kwamba maisha yanawaendea vyema, huku wakitumia mazingira haya kama ndoano ya kuwanasa vipusa hasa wanaojisimamia kifedha.

Mabinti wanaoangukia mitego ya aina hii hupigwa na butwaa baada ya muda mfupi wa kuchumbiana wanapokumbana na matamshi kama vile: “nikopeshe mapeni kidogo”, au “lipa bili nitakurejeshea senti”, wakidai wanasubiri hundi fulani.