Habari

'LOCKDOWN': Rais apuuza Joho

April 26th, 2020 2 min read

Na VALENTINE OBARA

RAIS Uhuru Kenyatta amepuuza mwito wa Gavana wa Mombasa Hassan Joho wa kuweka kafyu usiku na mchana jijini humo ili kuzuia maambukizi zaidi ya virusi vya corona.

Badala yake Rais Kenyatta alitangaza kuongezwa kwa muda wa siku 21 kwa kafyu ya usiku kote nchini, na marufuku ya kuingia na kutoka Mombasa pamoja na Nairobi, Kilifi, Kwale na Mandera

Bw Joho amekuwa akihimiza kafyu ya saa 24 Mombasa, akisema kuna haja ya kusitisha shughuli zote ili kuzima ueneaji wa Covid-19, kwani kaunti hiyo inageuka kuwa kitovu cha maambukizi.

Hapo Jumamosi baada ya kukutana na Rais Kenyatta katika Ikulu ya Nairobi, Bw Joho alisisitiza kwamba kutokana na yale anayoshuhudia Mombasa, kuna haja ya wakazi kukaziwa zaidi kwa kukosa nidhamu ya kufuata maagizo yanayotangazwa na serikali.

“Kutokana na yale tunayoshuhudia kwetu Mombasa, wakazi wanahitaji kuongezewa vikwazo. Atakayeumia kwa vikwazo hivyo ni mwananchi, lakini suluhisho pia liko mikononi mwa mwananchi akifuata masharti,” akasema Bw Joho.

“Idadi ya maambukizi inaongezeka katika kaunti yangu. Watu hawafuati masharti. Kama hujipendi wewe, kuna watu wanaokupenda…fuata maagizo kwa sababu yao,” akasema.

Lakini Rais Kenyatta alisita kukubali mwito wa Bw Joho. Hata hivyo alisema hatasita kutangaza hatua kali zaidi Pwani, iwapo hali ya maambukizi itakuwa mbaya zaidi Mombasa, Kilifi na Kwale.

Hapo Jumamosi Rais alifanya mkutano katika Ikulu na Bw Joho, Amason Kingi wa Kilifi na Salim Mvurya wa Kwale.

Viongozi hao walijadiliana kuhusu hatua ambazo zinafaa kuwekwa ili kukabiliana na ongezeko la idadi ya maambukizi katika kaunti hizo za kitalii.

Kufikia Jumamosi, idadi ya maambukizi kitaifa ilikuwa imefika 343 huku waliopona wakifika 98.

Katika hotuba yake kwa taifa, Rais Kenyatta alisema hatua yoyote kali itakayochukuliwa na serikali kuu itafanywa tu baada ya mashauriano na kaunti husika, pamoja na ushauri wa wataalamu wa matibabu.

Kulingana naye, serikali inatazamia kulegeza masharti hivi karibuni, lakini hilo litafanywa tu kama wataalamu wa afya watatoa hakikisho kwamba hakuna hatari ya watu kueneza maambukizi.

“Hatua ya kukaza au kulegeza kamba itachukuliwa kwa kuzingatia jinsi hali itakavyokuwa. Serikali ina nia ya kulinda maisha ya wananchi, kwa hivyo twataka kupunguza masharti lakini hatutasita kuyaongeza tukiona huu ugonjwa bado unaendelea kuenea hasa wakati huu tunapoingia kipindi cha baridi na mvua,” akasema Rais.

Kulingana na wataalamu wa masuala ya uongozi, si rahisi mataifa yanayoinuka kiuchumi kama Kenya kutekeleza agizo la kusitisha shughuli zote za eneo au taifa kutokana na umaskini wa idadi kubwa ya wananchi.

Agizo aina hii litahitaji serikali kutafuta jinsi ya kulisha maelfu ya watu, na ikikosa kufanya hivyo kuna uwezekano mkubwa wa utovu wa usalama hasa uporaji.

Hali kama hii tayari imeshuhudiwa Afrika Kusini, ambako Rais Cyrill Ramaphosa amelazimika kulegeza masharti baada ya vurugu kuongezeka hasa mitaa ya wananchi wenye mapato ya chini wanaotegemea vibarua.

Magavana Mvurya na Kingi waliepuka suala la masharti makali zaidi na badala yake wakashinikiza Wakenya kufuata maagizo ya serikali kama wanataka kuona hali ya kawaida ikirudi.

Bw Mvurya alieleza wasiwasi kuhusu jinsi Kaunti ya Kwale imepakana na Tanzania, ilhali idadi ya maambukizi inaongezeka sana katika nchi hiyo jirani.

Kwa upande wake, Bw Kingi alitaka kila mwananchi atambue masharti yanayowekwa ni kwa minajili ya kujilinda.

“Ni muhimu kila mwananchi awe na nidhamu kibinafsi. Unaweza kusukuma ng’ombe hadi mtoni lakini kunywa maji ni hiari yake. Ni aibu kubwa kwamba lazima askari wasimame mbele yetu ama viongozi wa serikali wawe karibu nasi ndipo tuvae maski au tunawe mikono,” akasema.

Rais Kenyatta alieleza matumaini kwamba janga la corona litaondokea nchi hivi karibuni.