Dondoo

Lofa aanguka akiiba sola kwa jirani

December 18th, 2019 1 min read

NA NICHOLAS CHERUIYOT

MERIGI, BOMET

Mlofa wa eneo aliomba msaada alipoanguka akijaribu kupanda paa la nyumba ya jirani kuiba mtambo wa sola.

Mdaku wa makala anasimulia kuwa mlofa alidhani kuwa mrembo mwenye boma hakuwa nyumbani na akaamua kujaribu bahati kuiba mtambo huo ambao amekuwa akitamani sana.

“Mwenye boma alikuwa ameondoka kwake asubuhi na akaingia wakati wa usiku na kulala moja kwa moja bila jamaa huyo ambaye alikuwa akifanya uchunguzi kwa ukaribu kumuona akirudi,” mdaku aliarifu.

Usiku wa manane, jamaa alianza hila yake kwa kunyata hadi nyumba hiyo na kisha akatumia ngazi kupanda juu paani tayari kung’oa mtambo.

“Mara ya kwanza niliposikia kuna adui nje, woga ulinikabili na sikupata hata nguvu ya kupiga mayowe. Nilitetemeka tu kitandani nikiloa jasho,” mrembo alielezea majirani siku iliyofuata.

Kelele paani mwa nyumba zilipozidi, mrembo alihofia huenda mwizi akavunja mabati kuingia ndani ya nyumba ndipo akapiga kamsa iliyomfikia jirani yake.

Lofa alishtuka kujua kulikuwa na mtu ndani na alipojaribu kushuka kasi alikosa mwelekeo na kubingirika hadi chini ambapo alipata jeraha la mguu huku akilia kwa sauti ya juu.

Jirani mmoja alikimbia na alipofika alimulika kwa tochi na kupata mlofa akigaragara chini kwa maumivu makali.

“Mwenye boma naye aliitwa atoke nje ajionee kioja na akabaki kinywa wazi kwani alimjua vizuri jamaa huyo aliyejaribu kumuibia,” mdokezi alituarifu.

Hatimaye, mlofa alifanyiwa huduma ya kwanza na uchungu ulipopungua akaomba kurudi kwake naye mrembo akabaki akiapa kumchukulia hatua za kisheria