Dondoo

Lofa alishwa viboko kwa kutelekeza mke

March 12th, 2018 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

IKOLOMANI, KAKAMEGA 

Kalameni mmoja wa eneo hili alijipata pabaya baada ya mashemeji zake kumuangushia viboko vikali.  Inadaiwa mashemeji wa polo walikasirishwa na hatua ya polo ya kuhamia kwa mpango wake wa kando na kumuacha dada yao akiteseka na watoto. 

Kulingana na mdokezi, mara kwa mara, polo hakuwa akipatikana kwake. Shughuli zake zote alifanyia kwa mpango wake wa kando.  Duru zinaarifu kwamba mkewe  aliamua kueleza mama mkwe na baba mkwe.

Alipoona hapati usaidizi wowote, aliamua kwenda kwao na kuwaeleza ndugu zake.

Inasemekana makalameni walighadhabishwa na tabia ya polo. Waliamua kuenda moja kwa moja hadi kwa nyumba ya kipusa aliyesemekana kuwa mpango wa kando wa polo.

Kulingana na mdokezi walipofika huko, walimpata polo pamoja na mrembo wakifurahia chajio.  “Bosi tunataka utuambie familia yako iko wapi?” makalameni walimuuliza polo. Polo aliwaeleza mashemeji waachane naye.

“Sijui ni shetani gani amewatuma kwangu. Huyu ni mke wangu wa pili. Kama kuna jambo acha niwapate kwa dada yenu tukazungumzie huko,” polo aliwakaripia mashemeji.

Mashemeji walianza pia kumkemea.  “Wewe ni mjinga sana. Huwezi kumuacha dada yetu akitaabika na watoto na unakuja hapa kula raha na huyu malaya,” makalameni walimkaripia polo.

Walipoona polo hakushtuka, mashemeji walichomoa viboko na kuanza kumwangushia polo.  Alipoona viboko vikimlemea, polo alichomoka mbio huku akiacha sima kwa kuku nyuma aliyokuwa amenunua.

Duru zinasema makalameni walimfuata  huku wakiendelea  kumuangushia viboko hadi nyumbani kwake.

Majirani wa polo walibaki midomo wazi huku wengine wakiwapongeza makalameni kwa hatua waliyoichukua.