Dondoo

Lofa azabwa makofi na ‘chips funga’

May 25th, 2020 1 min read

Na TOBBIE WEKESA

EMBAKASI, Nairobi

LOFA mmoja mkazi wa eneo hili aliangushiwa kichapo kikali demu wake alipogundua kwamba anamchukulia kama ‘chips funga’.

Inadaiwa tangu wawili hao waanze safari ya mapenzi, mrembo amekuwa akimhimiza polo wafunge pingu za maisha lakini jamaa anamkwepakwepa.

Duru zinasema siku ya tukio kidosho alimtembelea jamaa kwake na kumwambia kwamba ameamua anataka kuwa mke wake.

“Mimi sirudi kwetu. Nimekuja kuolewa!” binti alianza kumueleza lakini polo alimuangalia tu na kujitia hamnazo.

Kipusa aliendelea na kumfahamisha kwamba begi aliyokuwa amebeba ilikuwa na nguo zake na kwamba “sioni nikirudi kwetu hivi karibuni.”

Maneno ya kidosho yalimfanya kuzubaa kwa muda.

“Mimi siko tayari kukuoa sasa hivi. Nyumbani nina mke mwingine,” kalameni alifoka.

Mwanadada huyo akainuka kutoka kwenye kochi na kumsongea, jamaa akasonga.

“Mimi na wewe tulikuwa marafiki tu wa kawaida. Hatukuwa tumeafikiana kuoana,” akamuambia kwa ukali.

Kidosho alimtazama kwa uso na kusisitiza: “Mimi si mtoto mdogo. Kama hukuwa tayari kunipenda kikamilifu ungeniambia mapema badala ya kunitumia.”

Kabla ya polo kusema lolote alizabwa kofi.

“Uliniona mimi ni chips funga wa kununuliwa kando barabarani. Utanijua vizuri,” mwanadada akafoka.

Kalameni alijaribu kujinasua kutoka mikononi mwa kipusa lakini hakutoboa.

“Niachilie tutatue hili suala kwa amani,” polo alimrai.

Kipusa hakutaka kusikia lolote.

“Utachezea msichana mwingine lakini si mimi. Kila wiki nimekuwa nikija hapa kukitakasa kitanda chako halafu leo unaniambia ujinga,” demu alimkaripia jamaa huku akimuangushia teke.

Inadaiwa polo alipoona maji yamezidi unga aliamua kuwaita majirani.

“Huyu jamaa ni mjinga sana. Amerina asali yangu kwa muda mrefu halafu leo ananiambia hayuko tayari kunioa,” kidosho aliwaambia majirani.