Habari za Kitaifa

Lori lanaswa Kisii uchunguzi wa wizi wa vitabu ukichukua mkondo mpya

January 23rd, 2024 2 min read

NA BARNABAS BII

UCHUNGUZI kuhusu maboksi 540 ya vitabu vyenye thamani ya mamilioni vilivyopatikana katika msitu wa umma katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet, ulichukua mkondo mpya Jumanne, polisi wanaochunguza wizi huo walipopata malori mawili yenye nambari sawa za usajili.

Polisi walikamata lori moja mjini Kisii, lililokuwa na nambari sawa na lililotumika kusafirisha vitabu hivyo kutoka Moran Publishers hadi shuleni, Kaunti ya Nyamira.

Lori hilo, lenye rangi ya samawati, kinyume na lile jeupe lililopakiwa vitabu kabla ya kuondoka kwenye kampuni ya uchapishaji.

Kamanda wa Kaunti ya Elgeyo Marakwet, Bw Peter Mulinge, alisema maafisa wa upelelezi wanamfuatilia dereva huyo ambaye amezima simu yake baada ya kutupa vitabu vilivyokusudiwa kupelekwa kaunti ndogo za Nyamira Kaskazini na Nyamira Kusini.

“Tuko tayari kubaini jinsi vitabu hivyo viliishia kwenye msitu huo. Inakuwaje sadfa, nambari ya magari kufanana lakini lori tofauti na lililotumiwa kusafirisha vitabu hivyo,” alieleza Bw Mulinge.

Vitabu hivyo viligunduliwa vikiwa kando ya barabara ya Kaptagat-Kaptarakwa Jumapili iliyopita na wananchi waliomjulisha chifu wa eneo hilo, ambaye naye aliwaarifu polisi.

“Wachapishaji wamethibitisha kupewa kandarasi na kampuni moja ili kusafirisha vitabu hivyo hadi shule za Nyamira. Tutafuatilia video za CCTV, kubaini jinsi vitabu hivyo viliishia msituni huku msako wa kumtafuta dereva wa lori ukianza,” aliongeza Bw Mulinge.

Vitabu vilivyopatikana vilipelekwa katika kituo cha polisi cha Kaptagat huku shule zikifunguliwa kwa muhula wa kwanza.

Serikali iliyopita ilibadilisha mfumo wa usambazaji vitabu shuleni kwa nia ya kukabiliana na wizi huo na pia kuhakikisha usawa wa usambazaji.

Katika usambazaji huo mpya, serikali hununua vitabu moja kwa moja kutoka kwa wachapishaji ili kushughulikia ukosefu wa usawa. Wauzaji wa vitabu wakihisi kufungiwa nje ya msururu wa usambazaji.

Mwenyekiti wa Chama cha Wachapishaji Vitabu nchini, Bw Kamau Kiarie, amewataka wauzaji vitabu kuungana na kuwashirikisha wachapishaji ili kuwezesha usambazaji vitabu moja kwa moja shuleni.

Muungano huo, umekuwa ukikabiliana na uharamia na gharama ya juu ya uchapishaji wa vitabu, miongoni mwa changamoto zingine katika tasnia ya vitabu.