Habari Mseto

LSK kufika kortini ikitaka DCI akome kukamata washukiwa Ijumaa

December 31st, 2018 1 min read

Na SAM KIPLAGAT

CHAMA cha Wanasheria Nchini (LSK) sasa kinapanga kuwasilisha kesi mahakamani kupinga mtindo wa kukamatwa kwa washukiwa wa ufisadi siku za Ijumaa, kwa lengo la kuwazuilia korokoroni wikendi.

Akiongea na Taifa Leo kwa njia ya simu Rais wa LSK Allen Gichuhi alisema kesi yao pia itapendekeza kwamba washukiwa wawe wakipewa bondi ya polisi, haswa ikiwa hawajaonyesha dalili za kutoroka.

Kauli yake iliungwa mkono na Wakili mwenye tajriba ya juu Ahmednassir Abdullahi ambaye alikosoa kukamatwa kwa Wakili Tom Ojienda Ijumaa wiki jana.

Bw Abdullahi alisema hatua hiyo inatoa taswira mbaya kuhusu utendakazi wa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji na mwenzake wa Upelelezi wa Jinai (DCI) George Kinoti.

Wakili huyo alisema ni makosa kwani tangu kukamatwa kwa Profesa Ojienda Ijumaa, hakuna taarifa yoyote imeandikishwa kutoka kwake (Ojienda) ambaye ni mwanachama wa Tume ya Huduma za Mahakama (JSC).

“Mbona wasubiri hadi Ijumaa ndipo wamkamate mtu ambaye wamekuwa wakimchunguza kwa muda mrefu,” akauliza Bw Abdullahi baada ya kumtembelea Profesa Ojienda katika Kituo cha Polisi cha Muthaiga.

Alisema Profesa Ojienda alikuwa amewasilisha kwa polisi stakabadhi zote zinazohusiana na kesi zote kuhusu Kampuni ya Sukari ya Mumias ambazo aliwahi kushughulikia, kuondoa madai kwamba aliwasilisha kesi bandia kwa niaba ya kampuni hiyo.

Wakili huyo ndiye mtu mashuhuri wa hivi punde kukamatwa Ijumaa katika mtindo ulioanzishwa na polisi ili kuwapa nafasi ya kuwazuiliwa washukiwa kwa Zaidi ya saa 24 inayokubalika kisheria kabla ya kuwawasilisha kortini.

Mapema mwezi huu Bw Haji alitetea hatua ya kukamatwa kwa washukiwa siku za Ijumaa akisema hawezi kujutia hatua hiyo kwani ni “halali na haijakiuka sheria”.

“Hapo awali, polisi walikuwa wakiendeleza operesheni za kuwakamata washukiwa Ijumaa na hakuna aliyelalamika. Sasa mbona ikiwa watu wa hadhi ya juu ndio wanakamatwa, malalamishi yanaibuliwa?” Bw Haji aliuliza kwenye kikao na wanahabari mjini Naivasha.