Habari

LSK, mashirika yahimiza Rais avunje Bunge

September 25th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

USHAURI wa Jaji Mkuu David Maraga kwamba Rais Kenyatta anafaa kuvunja bunge kwa kutopitisha sheria ya kutekeleza usawa wa kijinsia, unaendelea kuibua mihemko huku wanasheria na mashirika zaidi ya kumi yakimuunga mkono.

Alhamisi, chama cha wanasheria Kenya (LSK), kilimpatia Rais Kenyatta hadi Oktoba 12 avunje bunge kikisema wabunge hawafai kuwa wakihudumu kufuatia ushauri wa Bw Maraga.

Mwenyekiti wa chama hicho, Bw Nelson Havi, alisema kuwa mshahara wa wabunge unafaa kusimamishwa, walinzi kuondolewa na ofisi zao katika maeneobunge kufungwa kufikia Oktoba 12.

“Baada ya tarehe hiyo, wabunge hawatakuwa kazini. Watakuwa wakivunja sheria kukanyaga majengo ya bunge na tutawazuia kufanya hivyo,” Bw Havi aliambia wanahabari jijini Nairobi.

Alikanusha kauli za wabunge kwamba kutakuwa na mzozo wa kikatiba bunge likivunjwa akisema sheria inapatia Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), siku 90 kufanya uchaguzi na watakaochaguliwa kuhudumu kwa kipindi kilichosalia.

“Hawa watu walikuwa na wakati wa kufanya kazi yao lakini walishindwa kufanya. Wanafaa kuondoka tuchague walio tayari kufanyakazi,” alisema.

Tume ya Huduma za Bunge (PSC) inayoongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa, Bw Justin Muturi, ilisema kwamba kutekeleza hitaji la usawa wa jinsia ni ghali mno. PSC ilisema bunge halina jukumu la kikatiba kupitisha sheria hiyo.

Bw Havi alisema kwamba vipindi vya kuhudumu vya Rais, magavana na madiwani haviathiriwi na ushauri wa Bw Maraga kwa rais.

Kauli ya LSK ilijiri saa chache baada ya mashirika 14 ya kutetea haki za wanawake kumuunga mkono Bw Maraga na kukashifu wabunge kwa kumshtumu. Mashirika hayo yalisema Bw Maraga alitekeleza jukumu lake la kikatiba baada ya wabunge kushindwa kupitisha sheria ya kutekeleza usawa wa jinsia kwa miaka kumi.

“Wanawake wa Kenya wanamuunga mkono Jaji Mkuu kwa kushauri Rais avunje bunge. Hatua ya Jaji Mkuu inafaa na inatambua changamoto zinazoendelea kukabili wanawake katika kutaka ushirikishi na usawa,” mashirika hayo yalisema kwenye taarifa ya pamoja.

Waliwataka wabunge kuheshimu katiba na utawala wa sheria.

“Tunatambua kwamba uamuzi wa Jaji Mkuu umefuatia bunge kushindwa kutoa mwelekeo wa kufanikisha usawa wa jinsia inavyohitaji katiba,” mashirika hayo yanasema.

“Bunge limeshindwa kufikia uamuzi na halijaonyesha nia njema wala heshima kwa utawala wa sheria,” i taarifa ya mashirika hayo iliongeza.

Pia yalisuta wabunge yakisema kwamba Bw Maraga hakukiuka sheria na ushauri wake kwa rais ni jukumu alilotwikwa na katiba.

“Msingi wa demokrasia ni kuheshimu utawala wa sheria na majukumu ya mihimili tofuati ya serikali,” yalisema na kuongeza kuwa yana imani Rais Kenyatta atatoa mwelekeo unaofaa kuhusu suala hilo.

Mashirika hayo yalisema hayo huku kesi mbili zikiwasilishwa katika Mahakama Kuu kupinga ushauri wa Bw Maraga. Katika kesi hizo, walalamishi wanataka mahakama iagize Rais asivunje bunge.

Baadhi ya mashirika yaliyotia sahihi taarifa hiyo ni Echo Network Africa, Common Women Agenda (COWA), Centre for Multiparty Democracy Kenya, Democracy Trust Fund, Africa Women Leaders Network (AWLN), Centre for Rights Education and Awareness (CREAWKenya), Kenya Female Advisory Organization (KEFEADO) na SDGs Kenya.