Habari Mseto

LSK yadai ufisadi umerejea Wizara ya Ardhi

September 1st, 2019 1 min read

Na GAKUU MATHENGE

JUHUDI zinazoendelea za kuteua makamishna wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) hazitakuwa na maana yoyote ikiwa utendakazi mbaya na ufisadi katika afisi kuu za wizara ya ardhi katika jumba la Ardhi, Nairobi, hazitakomeshwa, chama cha mawakili nchini LSK kimesema.

Matapeli wa zamani wamerejea katika Ardhi House huku ripoti za faili na stakabadhi ya umiliki wa ardhi kupotea zikiendelea kuripotiwa kila uchao.

Mpango wa utoaji hudumu kidijitali ulioanzishwa na Waziri wa Ardhi Farida Karoney unahujumiwa kupitia kukwama kila mara kwa mitambo na programu za kimtandao.

Kwa hivyo, maafisa wanaosimamia idara mbalimbali muhimu wangali wanaendelea kutumia stakabadhi kutoa hudumu hata wakati ambazo shughuli hizo zinaweza kuendeshwa kimtandao.

Hiyo ndiyo maana kulingana na Chama cha Mawakili Nchini (LSK) ulaghai bado unaendeshwa na maafisa wa ardhi kupitia visa vya “kupotea kwa faili”, ukiukaji wa sheria wakati wa usajili wa ardhi, na kuondolewa kiholela kwa ilani dhidi ya uuzaji wa ardhi.

“Usajili wa ilani za ardhi unachukua wiki nyingi, hali inayoweka wananchi kwenye hatari ya kupoteza mali au kulaghaiwa,” anasema mwenyekiti wa LSK Allen Gichuhi kwenye barua ya malalamishi aliyomwandikia Waziri Karoney. Kulingana na barua hiyo iliyotumwa na Bw Gichuhi mnamo Juni 26, 2019, LSK inalalamikia kukithiri kwa ufisadi, utepetevu, ulaghai, ukiukaji wa sheria na ongezeko la matapeli katika Ardhi House.

LSK inasema baadhi ya stakabadhi za umiliki wa ardhi zinahamishwa kutoka kwa afisi ya Msajili Mkuu wa Ardhi hadi afisi za maafisa kama hao katika ngazi za kaunti kisiri hali inayoibua maswali kuhusu uhalali wa baadhi ya stakabadhi hizo.