Habari Mseto

LSK yapinga kanuni za kuzima mikutano

October 12th, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

CHAMA cha wanasheria nchini (LSK) Jumatatu kiliwasilisha kesi katika Mahakama Kuu kupinga kanuni za Kamati ya Kitaifa ya Ushauri kuhusu Usalama (NSAC) kuhusu mikutano ya hadhara.

Kanuni hizo zilizoidhinishwa na Baraza la Mawaziri wiki iliyopita zinaingilia uhuru wa kujieleza ulio kwenye Katiba.

Katika kesi hiyo, LSK inaomba mahakama kuharamisha kanuni hizo.

Mawakili hao wanaiomba mahakama kushughulikiwa kesi hiyo kwa dharura ikitiliwa maanani kanuni hizo zinabagua na kukandamiza haki za wananchi.

LSK inasema kuwa kanuni hizo zinatumiwa vibaya na maafisa wa polisi.

Katika ushahidi uliowasilishwa mahakamani, Rais wa LSK Nelson Havi amesema kifungu nambari 5 cha Sheria za Udumishaji wa Utangamano kinakinzana na Katiba na chapasa kuharamishwa na mahakama.

Rais huyo wa LSK anasema kifungu hiki kinatumiwa kukandamiza haki na uhuru wa wananchi wa kutangamana, kutoa maoni, kufanya mikutano ya hadhara, na kuwazuia watu fulani kuhutubia mikutano ya kisiasa.

Bw Havi anasema ombi kuu la LSK ni kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai ama afisa mwingine yeyote wa polisi wazimwe kutumia mamlaka yao vibaya.

Kulingana na Bw Havi, polisi hawapasi kutumiwa kuvuruga mikutano ya wanasiasa, ama maandamano huku akirai mahakama kuu ipige kalamu maagizo hayo ya NASC.

Chama cha LSK kimepanga kuvamia ya Bunge kwa lengo la kumshurutisha Rais Uhuru Kenyatta atekeleze ushauri wa Jaji Mkuu David Marag kuwa avunje bunge kwa kushindwa kutunga sheria ya jinsia.

Bw Havi anaomba korti imuru polisi wasithubutu kuvuruga mkutaano huo wa mawakili ama kuwatawanya.

Kwa mujibu wa kanuni za NSAC, anayeomba idhini ya kufanya mkutano anatakiwa kuhudhuria mkutano wenyewe kwa lengo la kuwasaidia maafisa wa usalama kudumisha amani na utangamano.

Wanaoitisha mikutano hiyo lazima wamjuluishe afisa mkuu wa polisi ama afisa mwingine yoyote anayehusika na masuala ya usalama.