Habari Mseto

LSK yataka majaji wapya kabla 2021

November 1st, 2020 2 min read

Na CHARLES WANYORO

CHAMA cha Wanasheria Nchini (LSK) sasa kinataka mchakato wa kuteua Jaji Mkuu mpya usitishwe.Badala yake LSK inataka juhudi hizo zielekezwe katika uteuzi wa majaji 41 walioidhinishwa na Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) mwaka 2019.

Jaji Mkuu David Maraga anastaafu Januari mwaka ujao. Rais wa LSK Nelson Havi pia anataka uteuzi wa Jaji wa Mahakama ya Juu atakayejaza nafasi ya Jaji Jackton Ojwang’, ambaye tayari amestaafu, usitishwe.

Bw Havi alitishia kuongoza maandamano ya mawakili kumshinikiza Rais Uhuru Kenyatta kuteua majaji hao, akisema kucheleweshwa kwa shughuli hiyo kumechangia mrundiko wa kesi mahakamani.

“Tuna majaji 41 walioidhinishwa na JSC ili kuteuliwa rasmi na Rais, lakini hilo halijafanyika baada ya mwaka mmoja. Ikiwa hatuna majaji basi ujenzi unaoendelea wa mahakama zaidi hautakuwa na maana yoyote. Ndiposa napendekeza tuandamane barabarani kushinikiza uteuzi ufanywe,” akasema jana mjini Meru.

Bw Havi ambaye aliandamana na naibu wake Carolyn Kamende, mwenyekiti wa LSK ukanda wa Mlima Kenya Linda Koome na maafisa wengine, alisema hayo alipoongoza hafla ya kufungua ofisi kuu ya LSK eneo hilo.

Rais huyo alihoji kwamba wanasheria wanahisi kucheleweshwa kwa uteuzi wa majaji ni njama ya Ofisi ya Rais kuingilia na kuhujumu utendakazi wa Idara ya Mahakama.

“Haja yetu ni kuona majaji hao wapya wameanza kazi haraka iwezekanavyo ili kusikiza kesi nyingi zilizokwama mahakamani,” Bw Havi akasema.Jaji Mkuu Maraga, ambaye pia ni Rais wa JSC, anatarajiwa kustaafu mnamo Januari 12 baada ya kuhitimu umri wa miaka 70 kulingana na matakwa ya Katiba.

Bw Maraga anatazamiwa kwenda likizo ya mwisho kuanzia Desemba 12 mwaka huu kusubiri kustaafu. Kwa mujibu wa sheria utaratibu wa kujaza nafasi hiyo unapasa kuanza baada ya Januari 12, 2021.

Lakini JSC inataka Bunge kufanyia sheria hiyo marekebisho ili shughuli ianze mapema kuzuia uwezekano wa kuwepo kwa mwanya katika uongozi wa Idara ya Mahakama.

Ikizingatiwa kuwa Jaji Ojwang’ alistaafu mwaka huu, kuondoka kwa Maraga kutamaanisha Mahakama ya Juu itasalia na majaji watano pekee – hali ambayo inaweza kutatiza utendakazi wake endapo mmoja wa majaji waliosalia atakosekana kwa sababu moja au nyingine.

Kuhusu ripoti ya BBI, Bw Havi aliwaambia mawakili kutafakari ikiwa Idara ya Mahakama itasalia huru iwapo idadi ya wawakilishi wa majaji na mawakili katika JSC itapungua, ili kubuniwe wadhifa wa afisa atakayekuwa akipokea malalamisha kuhusu majaji, maarufu “Judiciary Ombudsman”.

Kiongozi huyo wa LSK pia alidai kuwa kuna mpango wa kuhujumu Mahakama hata zaidi kwa kupunguza mgao wake wa fedha kutoka kwa bajeti ya taifa.

“Kwa mfano, Hazina ya Kitaifa imefeli kuitenga Sh500 milioni zilizotarajiwa kufadhili mpango wa kugeuza rekodi za mahakama hadi mfumo wa digitali,” akaongeza.