Habari

Lugha asili zina umuhimu mkubwa katika ustawi wa taifa – mtaalamu

August 6th, 2019 1 min read

Na WANDERI KAMAU

MTAALAMU amesema ni muhimu lugha asili zikazingatiwa nchini hasa wakati huu ambapo taifa limeanza kutumia mfumo wa uamilifu, Competency Based Curriculum (CBC).

Bingwa huyo wa lugha amesema uzingatiaji wa lugha asili ndiyo njia pekee itakayohakikisha kufaulu kwa Mfumo Mpya wa Elimu wa 2-6-6-3.

Akihutubu Jumanne asubuhi kwenye kongamano maalumu kuhusu uzingatiaji lugha katika masomo katika Taasisi ya Kutengeneza Mitaala nchini Kenya (KICD), mtaalamu wa lugha, Prof Nathan Ogechi amesema kuwa Kenya haijapiga hatua zifaazo kimasomo kwa kutozingatia lugha hizo.

Msomi huyo amesema kuwa lazima mfumo huo uzibe pengo la mfumo wa 8-4-4 ambao ulitia maanani matumizi ya Kiingereza kama lugha ya mawasiliano.

“Nchi nyingi zilizostawi kiviwanda zimekuwa zikikuza lugha zao asili kwa kutambua umuhimu wake, hasa katika kuchangia ukuaji wa kiuchumi na mshikamano miongoni mwa wanajamii,” amesema Prof Ogechi.

Kaulimbiu ya kongamano hilo ni ‘Kupanua Ujumuishaji: Kuhamasisha Mafunzo kupitia Lugha katika Karne ya 21’.