Michezo

Luis Garcia kuhudhuria fainali za Chapa Dimba

June 18th, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

MWANASOKA mstaafu aliyewahi kuzipigia klabu za Liverpool na Barcelona bila kusahau Atletico Madrid, winga Luis Javier Garcia ameratibiwa kuhudhuria fainali za kitaifa za Chapa Dimba na Safaricom Season Two mwaka huu.

Mstaafu huyo ameteuliwa kuwa balozi wa LaLiga kwenye mechi hizo zitakazokunjua jamvi Alhamisi hii na kukamilika Jumamosi katika Uwanja wa kinoru Stadium, Kaunti ya Meru. Mechi hizo zitajumuisha timu nane za wavulana na saba za wasichana kutoka maeneo nane kote nchini.

Timu itakayoibuka bingwa kwa wavulana pia wasichana kila moja itatuzwa cha Sh 1 milioni na wafadhili wakuu kampuni ya Safaricom. Mstaafu huyo ambaye ni raia wa Uhispania anayejivunia kushiriki mechi 150 kwenye ngarambe ya La Liga na kufunga magoli 22 atashauriana na chipukizi wa timu hizo hasa jinsi ya kupaisha talanta zao katika soka.

”Tuna furaha tele baada ya kupanua ushirikiano wetu na LaLiga na kutoa nafasi kwa mstaafu huyo kuhudhuria fainali za makala ya mwaka huu. Ningependa kutoa mwito kwa chipukizi watakaohudhuria mechi hizo kutumia fursa hiyo kujifunza mambo kadhaa ya kutoka kwa mstaafu huyo,” mkuu wa wateja wa Safaricom, Sylvia Mulinge alisema.

Kipute cha Chapa Dimba na Safaricom Season Two kilichoshirikisha takribani timu 1,600 kote nchini kilianza mwaka uliyopita kwa mechi za mashinani.