Luis Nani ajiunga na klabu ya Venezia

Luis Nani ajiunga na klabu ya Venezia

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Manchester United, Luis Nani, 35, amejiunga na kikosi cha Venezia kinachoshiriki Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Nyota huyo aliyechezea Man-United mara 230 kati ya 2007 na 2015 ameingia katika sajili rasmi ya Venezia kwa mkataba wa miezi 18. Alifunga mabao 41 na kuchangia mengine 73 katika kipindi hicho cha miaka minane ndani ya jezi za Man-United.

Kufikia sasa, Venezia wanakamata nafasi ya 17 kwenye msimamo wa jedwali la Serie A na wanakodolea macho hatari ya kuteremshwa ngazi ligini mwishoni mwa kampeni za msimu huu wa 2021-22.

Nani anajivunia kunyanyua taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na Europa League. Amewahi pia kutwaa mataji manne ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na matatu ya Ligi Kuu ya Ureno akichezea Sporting Lisbon.

Alichezea Sporting kwa kipindi kifupi baada ya kuondoka Man-United kisha akajiunga na Fenerbahce ya Ligi Kuu ya Uturuki mnamo 2015.

Sogora huyo amewahi pia kuvalia jezi za Valencia, Lazio na Orlando katika Major League Soccer (MLS).

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

AFCON: Salah abeba Misri dhidi ya Guinea-Bissau katika...

Timbe aongoza Buriram kurukia uongozi wa Ligi Kuu Thailand

T L