Michezo

Lukaku afunga bao la 18 msimu huu

June 22nd, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

ROMELU Lukaku alifunga bao lake la 18 kwenye Ligi Kuu ya Italia (Serie A) msimu huu katika mechi iliyowashuhudia waajiri wake Inter Milan wakiwacharaza Sampdoria 2-1 mnamo Juni 21, 2020.

Lukaku ambaye ni fowadi wa zamani wa Everton na Manchester United, alivurumisha kombora kutoka hatua ya 10 nje ya lango la Sampdoria na kusherehekea goli lake kwa kupiga goti kama ishara ya kuunga maandamano dhidi ya ubaguzi wa rangi.

Lautaro Martinez anayewindwa na Barcelona alifanya mambo kuwa 2-0 kutokana na krosi ya Lukaku kunako dakika ya 33 kabla ya Morten Thorsby kuwarejesha Sampdoria mchezoni katika dakika ya 52.

Ushindi kwa Inter uliwapaisha hadi nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 57, sita nyuma ya mabingwa watetezi Juventus wanaodhibiti kilele.

Kampeni za Serie A zilirejelewa mnamo Juni 20 baada ya kuahirishwa kwa muda mnamo Machi 9, 2020 kutokana na janga la corona.