Michezo

Lukaku afunga mabao mawili na kusaidia Inter kuinyuka Benevento ligini

October 2nd, 2020 1 min read

Na MASHARIKI

ROMELU Lukaku alifunga mabao mawili na kusaidia Inter Milan kuendeleza mwanzo bora katika kampeni za Ligi Kuu ya Italia (Serie A) msimu huu.

Mabao hayo ya Lulaku yaliwezesha waajiri wake, chini ya mkufunzi Antonio Conte, kuipepeta Benevento 5-2 mnamo Septemba 30, 2020.

Lukaku aliwafungulia Inter ukurasa wa mabao katika dakika ya kwanza baada ya kushirikiana vilivyo na Achraf Hakimi. Roberto Gagliardini na Lukaku walifanya mambo kuwa 3-0 kufikia dakika ya 28 kabla ya Gianluca Caprari kuwarejesha Benevento mchezoni kunako dakika ya 34.

Ingawa hivyo, Inter walionekana kuwazidi maarifa wenyeji wao katika kila idara na Hakimi akawafungia Inter goli la nne mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Alexis Sanchez alimwandalia Lautaro Martinez krosi safi katika dakika ya 71 na kuwapa Inter bao la tano kabla ya Caprari kufunga la pili kwa upande wa Benevento katika dakika ya 76.

Ushindi wa Inter unamaananisha kwamba kikosi hicho kwa sasa kimetawala mechi mbili za mwanzo wa msimu huu ligini kwa idadi kubwa ya mabao. Inter waliibuka na ushindi wa 4-3 dhidi ya Fiorentina katika mchuano wa ufunguzi wa kampeni za Serie A muhula huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO