Michezo

Lukaku afunga mawili na kuweka hai matumaini ya Inter Milan kufuzu kwa hatua ya 16-bora UEFA

December 2nd, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

ROMELU Lukaku alifunga mabao mawili na kusaidia Inter Milan kuweka hai matumaini ya kufuzu kwa hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kutoka Kundi B baada ya ushindi wa 3-2 dhidi ya Borussia Monchenglabach ya Ujerumani.

M’gladbach wangalifuzu kwa hatua hiyo ya mwondoano kwa kujipa uhakika wa kuwa viongozi wa kundi lao iwapo wangalibwaga Inter inayonolewa na kocha wa zamani wa Chelsea, Antonio Conte.

Hata hivyo, alama tatu sasa ndizo zinazotenganisha viongozi wa kundi M’gladbach na Inter wanaovuta mkia kwa pointi tano. Kila kikosi kimesalia na mchuano mmoja zaidi wa kusakata kundini.

Ingawa Matteo Darmian aliwaweka Inter uongozini katika dakika ya 17, juhudi zake zilifutwa na Alassane Plea aliyesawazsisha mambo mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Lukaku alifunga mara mbili chini ya dakika tisa za kipindi cha pili na kufanya mambo kuwa 3-1 kabla ya Plea kufunga la pili kwa upande wa M’gladbach katika dakika ya 75.

Kulitokea kizaazaa mwishoni mwa kipindi cha pili baada ya Ashley Young kukosa fursa nzuri ya kufungia Inter huku teknolojia ya VAR ikimnyima Plea fursa ya kufunga mabao tatu katika gozi hilo.

Katika mchuano mwingine wa Kundi B, mabingwa mara 13 Real Madrid walipepetwa 2-0 na Shakhtar Donetsk na kufanya kundi hilo kuwa wazi kwa mshindani yeyote kusonga mbele. Real kwa sasa watakuwa wenyeji wa M’gladbach katika mchuano wao wa mwisho kundini huku Shakhtar wakiwaendea Inter uwanjani San Siro, Italia mnamo Disemba 9, 2020.

Licha ya kujivunia nafasi ya pili kwenye kampeni za Ligi Kuu ya Italia (Serie A), Inter wamejizolea alama mbili pekee kutokana na mechi nne za ufunguzi wa kivumbi cha UEFA.

Inter walijibwaga ugani dhidi ya M’gladbach wakiwa na ulazima wa kushinda ili kuweka hai matumaini finyu ya kutinga hatua ya 16-bora ya UEFA kwa mara ya kwanza tangu 2012.