Michezo

Lukaku awapa Ubelgiji tiketi ya fainali za Uefa Nations League

November 19th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

ROMELU Lukaku alifunga mabao mawili na kusaidia Ubelgiji kufuzu kwa fainali za UEFA Nations League baada ya ushindi wa 4-2 dhidi ya Denmark mnamo Novemba 18, 2020.

Youri Tielemans wa Leicester City aliwafungulia Ubelgiji ukurasa wa mabao kunako dakika ya tatu kabla ya Denmark kusawazishiwa na Jonas Wind katika dakika ya 17.

Hata hivyo, Lukaku anayechezea Inter Milan ya Italia, alishirikiana vilivyo na kiungo wa Manchester City, Kevin De Bruyne na kufungia Ubelgiji goli la tatu katika dakika ya 57 kisha jingine katika dakika ya 69.

Nacer Chadli alijifunga katika ya 86 na kuwapa Denmark bao la pili sekunde chache kabla ya De Bruyne kuzamisha kabisa chombo cha Denmark waliokuwa wakichezea ugenini.

Ushindi kwa Ubelgiji wanaotiwa makali na kocha wa zamani wa Everton, Roberto Martinez unamaanisha kwamba Ubelgiji wanafuzu kwa fainali zijazo za Nations League baada ya kukamilisha kamilisha kampeni za makundi kileleni mwa Kundi A2. Ubelgiji walijibwaga ugani kwa minajili ya mechi dhidi ya Denmark wakijivunia motisha ya kupepeta Uingereza 2-0 katika gozi la awali mnamo Novemba 15, 2020.

Ubelgiji kwa sasa wanaungana na Ufaransa, Uhispania na Italia kwenye fainali za UEFA Nations League zitakazoandaliwa Oktoba 2021.

MATOKEO YA UEFA NATIONS LEAGUE (Novemba 18):

Bosnia 0-2 Italia

Poland 1-2 Uholanzi

Ugiriki 0-0 Slovenia

Kosovo 1-0 Moldova

Ubelgiji 4-2 Denmark

Uingereza 4-0 Iceland

Austria 1-1 Norway

N. Ireland 1-1 Romania

Czech 2-0 Slovakia

Israel 1-0 Scotland

Hungary 2-0 Uturuki

Serbia 5-0 Urusi