Michezo

Lukaku azidi kuwika katika Serie A

October 25th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

ROMELU Lukaku aliendeleza ubabe wake kwenye kampeni za msimu huu kwa kufunga bao na kuongoza waajiri wake Inter Milan kuwapepeta Genoa 2-0 kwenye Ligi Kuu ya Italia (Serie A) mnamo Oktoba 24, 2020.

Lukaku kwa sasa amepachika wavuni jumla ya mabao 15 kutokana na mechi 13 zilizopita akivalia jezi za Inter na timu ya taifa ya Ubelgiji. Isitoshe, anajivunia kufunga magoli 10 kutokana na mechi tisa za hadi kufikia sasa muhula huu.

Inter walikosa kuelekeza mpira wowote uliolenga shabaha langoni mwa wapinzani katika kipindi cha kwanza kwa mara ya kwanza tangu Machi 2019.

Bao lililofungwa na Lukaku katika dakika ya 64 lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na kiungo Nicolo Barella ambaye pia alichangia goli la pili ambalo Inter walifungiwa na fowadi Danilo D’Ambrosio.

Andrea Ranocchia alipoteza nafasi nyingi za wazi ambazo vinginevyo, zingewapa Inter mabao matatu muhimu mwishoni mwa kipindi cha pili.

Chini ya kocha Antonio Conte, Inter wamejizolea alama 10 kutokana na mechi tano zilizopita msimu huu na ni pengo la pointi mbili pekee linalowatenganisha na viongozi wa jedwali AC Milan.

Ushindi uliovunwa na Inter uliwasaidia kuwaruka Atalanta waliopokezwa kichapo cha 3-1 kutoka kwa Sampdoria kwenye uwanja wao wa nyumbani.