Michezo

Lukaku na Sanchez wasaidia Inter Milan kutoka nyuma na kupepeta Torino kwenye Serie A

November 23rd, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

ALEXIS Sanchez na Romelu Lukaku walicheka na nyavu za wapinzani katika dakika 26 za mwisho wa kipindi cha pili na kusaidia Inter Milan kutoka nyuma kwa 2-0 na hatimaye kupepeta Torino 4-2 kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A) mnamo Novemba 22, 2020.

Nyota wa zamani wa West Ham United, Simone Zaza aliwaweka Torino kifua mbele mwishoni mwa kipindi cha kwanza kabla ya Cristian Ansaldi kufunga la pili katika dakika ya 62.

Ingawa hivyo, Inter walirejea mchezoni kupitia kwa Sanchez katika dakika ya 64 kabla ya Lukaku kupachika wavuni magoli mawili kunako dakika za 67 na 84. Bao la pili la Lukaku yalichangiwa na Sanchez ambaye ni fowadi wa zamani wa Barcelona, Arsenal na Manchester United.

Goli la pili lililofungwa na Lukaku ambaye pia amewahi kuchezea Everton na Man-United lilitokana na penalti iliyochangiwa na mvamizi Lautaro Martinez aliyezamisha kabisa chombo cha Torino mwishoni mwa kipindi cha pili.

Ushindi wa Inter uliwapaisha hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali kwa alama 15, tatu zaidi nyuma ya viongoz Sassuolo. AC Milan wanashikilia nafasi ya tatu kwa alama 17 sawa na AS Roma wanaowazidi nambari nne Juventus kwa pointi moja pekee.

MATOKEO YA SERIE A (Novemba 22, 2020):

Inter Milan 4-2 Torino

Fiorentina 0-1 Benevento

Roma 3-0 Parma

Sampdoria 1-2 Bologna

Verona 0-2 Sassuolo