Makala

LuLu Hassan akiri kuangukia mume wa kishua, Rashid Abdallah  

April 8th, 2024 2 min read

NA SINDA MATIKO

NI zaidi ya miaka 15 tangu watangazaji maarufu wa runinga Rashid Abdallah na Lulu Hassan walipootesha penzi lao Mombasa wakiwa hawana chochote.

Sasa hivi, mastaa hao wanaishi maisha ya kutamaniwa na wakiwa wanaingiza mikwanja ya maana kupitia dili za matangazo ya kibiashara, mishahara yao kama watangazaji maarufu na mkwanja kupitia biashara ya utengenezaji filamu kupitia kampuni yao ya Jiffy Pictures.
Lulu anasema kila anapoitathmini safari yao, pamoja na mafanikio yao, moja ya mafanikio makubwa kwake ni kumpata Rashid Abdallah kama mume.

“Kikweli najionea fahari sana mume wangu. Ni moja kati ya mafanikio makubwa katika maisha yangu. Huwa halali nikizungumzia suala la uandaaji filamu. Yeye ndiye mbunifu wa shoo zote zetu ambazo tumeandaa, tukaingiza sokoni na zikafanya vizuri. Wakati mwingine huwa namhurumia kwa jinsi ambavyo yeye hujituma sana kazi. Ila kwa upande mwingine huwa naona kweli hapa nilimpata mume wa kishua,” anasema Lulu.
Kwa sasa, Jiffy Pictures inatamba na telenovela ya Zari iliyoingizwa sokoni miezi sita iliyopita.

Tayari kampuni ya Multi Choice imeidhinisha uaandaji wa Makala ya Pili ya Zari kuanza baada ya kupata mafanikio makubwa ya utazamaji.

Lulu anasema mafanikio ya Zari yamechangiwa na vitu viwili.

“Kwanza, tulibadilisha uandishi wetu sio kama zamani. Ukitizama Zari kwa makini utagundua utofauti ninaouzungumzia. Sasa hivi, hatuiburuzi stori sana maana watazamaji huishia kuchoka. Tunagonga tukio tukisonga. Mabadiliko haya ni baadhi ya majibu mitazamo tuliyokusanya  mitandaoni kutoka kwa mashabiki,” anasema Lulu.
Lakini sababu ya pili ya kufanikiwa kwa Zari ni wahusika waliowatumia.
“Wahusika wa Zari wanapendwa sana na mashabiki, ni watu wanaopendwa na watu wengi. Hawa ni watu ambao siku zote kama maprodusa, utataka kuwa karibu nao maana kama wanapendwa na watu, basi watu hao watataka kuwatazama ukiwaweka kwenye shoo,” anaelezea.

Lulu Hassan na mumewe, Rashid Abdallah, kwa sasa ni watangazaji katika runinga ya Citizen, inayomilikiwa na Royal Media Services.

Wanandoa hawa hupeperusha habari wakiwa pamoja kwa lugha sanifu ya Kiswahili.