Habari Mseto

LULU WILSON: Ni mlima lakini nitamfikia Lupita Nyong'o

March 13th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

ANAWATAKA wanawake wajiheshimu pia watambue malengo yao katika tasnia ya uigizaji vile vile wakomeshe kukubali kushushwa hadhi na wanaume.

Anashauri wasiwe kukubali matakwa ya maprodyuza mafisi ambao huwalazimishe kuingia katika mahusiano ya kimapenzi ili apewe ajira.

Pia anawahimiza kuwa nyakati zote wasitegemee kuajiriwa mbali waelewe ni muhimu kuwekeza katika biashara badala ya kuketi vijiweni kusubiri ajira.

Binafsi amepania kutinga kiwango cha kimataifa ikiwezekana kuwapiku wasanii mahiri kama Lupita Nyong’o kati ya Wakenya wanaofanya kweli katika muvi za Hollywood.

Ni kati ya waigizaji wanaoendelea kuvumisha sekta hiyo nchini huku akijivunia kushiriki filamu nyingi tu na kuonyesha kupitia runinga tofauti ikiwamo Citizen TV, Africa Magic na K24 miongoni mwa zingine.

Tunayezungumzia siyo mwingine mbali ni Lulu Wilson mwigizaji pia mfanyi biashara wa samaki kupitia mtandao ambapo hujulikana kama ‘Lulus Kitchen.’

Dada huyo alianza kujituma kwenye masuala ya uigizaji mwaka 2011 ambapo tayari anajivunia kunasa tuzo ya ‘Best Supporting TV Series Actress.’

‘Nilitwaa tuzo hiyo baada ya kufanya vizuri kwenye filamu iliyoitwa ‘Keru’ iliyokuwa ikirushwa kupitia K24 Televisheni,” alieleza na kuongeza kuwa anaamini ana uwezo tosha kubeba tuzo nyingi siku sijazo. Lulu aliyetambua kipaji chake akiwa mwanafunzi katika shule ya Upili ya Asumbi alishiriki filamu hiyo chini ya Zamaradi Productions. Pia aliwahi kufanya kazi na kundi la Still Works.

Binti huyu pia anajivunia kushiriki filamu za TV-Series za kipindi cha Papa Shindarula ambacho huonyeshwa kupitia Citizen TV. Aidha amekuwa akihusika katika filamu za ‘Viusasa’ kipindi cha Tichtek ta ambazo hurushwa kupitia kituo hicho. Kadhalika alishiriki filamu zingine kama ‘My Two Wives,’ na ‘Sense Eight’ ambayo huonyeshwa kupitia Netflix.

Kando na hayo hushiriki matangazo ya kibiashara katika vituo vya redio ambavyo hutangaza kwa lugha ya mama ‘Dholuo.’

Katika biashara huwa anauza samaki wa kukaranga aina ya ‘Omena’ na ‘mbuta -Nile perch.’ ”Biashara imenipiga jeki pakubwa hasa wakati sina ajira mahali popote,” alisema na kudokeza kuwa katika mpango mzima amepania kumiliki brandi ya kutengeneza filamu miaka ijayo ili kutoa nafasi za ajira kwa waigizaji chipukizi.

”Nawaambia wenzangu kwamba ni vyema wawe wakifanya kazi yao kadiri ya uwezo wao ili kutoa fursa nzuri kwa wahusika kuwaita tena ajira zinapotokea.

Pia wasanii chipukizi wawe wepesi kukosolewa ili kujifunza zaidi kuhusu uigizaji,” alieleza. Anashauri waliowatangulia waache kuwavunja moyo wasanii chipukizi maana baadhi yao hupenda kutumia jasho ya wenzao kujinufaisha.