Lungu adai kura ya urais ilijaa dosari mpinzani akiongoza

Lungu adai kura ya urais ilijaa dosari mpinzani akiongoza

Na Mashirika

RAIS wa Zambia, Edgar Lungu, amedai kuwa uchaguzi wa urais nchini humo ulikumbwa na dosari chungu nzima.

Alitoa madai hayo huku matokeo yakionyesha mpinzani wake, Hakainde ‘HH’ Hichilema, anaongoza katika kura zilizohesabiwa.

Lungu alisema maafisa wa chama chake cha Patriotic Front (PF) walifurushwa kutoka vituo vya uchaguzi, na hivyo waliacha karatasi za kura bila ulinzi.

Lakini Hichilema alijibu kwamba tetesi za rais huyo ni dalili za mwisho za serikali inayoondoka mamlakani.

Lungu alidai ghasia katika mikoa aliyoshindwa zilifanya uchaguzi kukosa uadilifu. Alisema chama chake kinawazia hatua ya kuchukua.

Tume ya uchaguzi ya Zambia haikujibu madai ya rais huyo, anayetafuta uongozi kwa muhula wa pili.Lungu alisema kwenye taarifa kwamba ghasia zilizuka katika mikoa ya kusini, kaskazini na magharibi.

Alitoa mfano wa kifo cha mwenyekiti wa PF mkoa wa magharibi na mwanaharakati wa chama hicho mapema mwezi huu, akisema ni ghasia ambazo ziliathiri uchaguzi.

Wachunguzi wa Muungano wa Ulaya (EU) walisema kura hizo zilikosa usawa katika kampeni, haki ya kukusanyika ilikandamizwa, na serikali kutumia vibaya mamlaka.

Mitandao ya kijamii na Intaneti ilizimwa Alhamisi lakini Ijumaa, Mahakama Kuu jijini Lusaka ikaagiza ifunguliwe.

You can share this post!

TAHARIRI: Wanaotoa chanjo watoe habari zote

Sitishwi na jeshi la wanaonipinga – Ruto