Habari

Lusaka achapisha rasmi notisi ya seneti kujadili hatima ya Sonko

December 7th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

SPIKA wa Seneti Ken Lusaka amechapisha kwenye gazeti rasmi la serikali notisi ya kikao maalum cha maseneta alichoitisha kushughulikia mashtaka yaliyomo kwenye hoja ya kumtimua afisini Gavana wa Nairobi Mike Sonko.

Kulingana na notisi hiyo iliyochapishwa mnamo Desemba 7, 2020, kikao hicho kitaanza saa nane na nusu alasiri Jumatano, Novemba 8, 2020, katika ukumbi wa mijadala ya maseneta katika majengo ya bunge, Nairobi.

Shughuli ya kipekee itakayoshughulikiwa siku hiyo ni mfumo ambao maseneta watatumia kusikiliza na kufanya maamuzi kuhusu mashtaka yaliyosababisha madiwani wa Kaunti ya Nairobi kupitisha hoja ya kumtimua afisini Alhamisi, Desemba 3, 2020.

Bunge la Kaunti hiyo lilimtimua Bw Sonko baada ya madiwani 88 kati ya 122 kuunga mkono hoja iliyowasilishwa na kiongozi wa wachache, Michael Ogada.

Bw Lusaka alisema ametoa ilani hiyo kwa maseneta kulingana na sheria za bunge la seneti nambari 30 (1) na ombi lililowasilishwa na Kiongozi wa Wengi Samuel Poghisio lililoandamanishwa na sahihi za angalau maseneta 15.

“Pia nimetoa notisi hiyo baada ya kupokea arifa kutoka kwa Spika wa Bunge la Kaunti ya Nairobi mnamo Desemba 4, 2020, ikiniarifu kuhusu kupitishwa kwa hoja ya kumwondoa afisini Gavana wa Nairobi, Mike Mbuvi Sonko,” akasema.

Spika Lusaka alisema maseneta watashughulikia suala hilo pekee siku hiyo na baadaye Seneti itaahirisha vikao vyake hadi Jumanne, Februari 9, 2021, saa nane na nusu alasiri, kulingana na kalenda ya Seneti.

Wengi wa madiwani walipiga kura kwa njia ya mtandaoni wakati wa kikao hicho cha Alhamisi wiki jana baada ya mjadala kuhusu hoja hiyo. Ni madiwani wawili pekee waliopinga hoja hiyo.

Kulingana na hoja hiyo, Bw Sonko aliondolewa mamlakani kwa matumizi mabaya ya mamlaka ya afisi yake, mienendo mibaya, kudinda kuidhinisha bajeti iliyotengewa Idara ya Huduma za Jiji la Nairobi (NMS) ya Sh27.7 bilioni na kutokuwa na uwezo kimwili na kiakili kuendesha shughuli za serikali ya kaunti hiyo.