Lusaka akiri kuwa katika uhusiano wa kimapenzi na aliyemshtaki

Lusaka akiri kuwa katika uhusiano wa kimapenzi na aliyemshtaki

Na Joseph Wangui

SPIKA wa Bunge la Seneti Kenneth Lusaka amekiri kuwa katika uhusiano wa kimapenzi na mwanamke ambaye aliekea kortini akitaka alipwe Sh25 milioni na mwanasiasa huyo ili kutunza mimba yake.

Jana, Mahakama ya Milimani iliruhusu Bw Lusaka na aliyekuwa mpenziwe Irene Naswa Mutaki ambaye ana mimba ya miezi mitatu kutatua suala hilo nje ya mahakama kisha kurejea kortini baada ya mwezi moja.

Bi Mutaki alikuwa ameelekea kortini akidai kwamba Bw Lusaka amemtelekeza na akataka amlipe kiasi hicho kikubwa cha pesa kutunza mimba yake na kuhudhuria vipimo vya kliniki.

Mbele ya Jaji Anthony Mirima, wakili wa Bw Lusaka Peter Wanyama aliirai korti kuwa wapewe siku 30 kumaliza mazungumzo kuhusu suala hilo kisha warejee kortini kunakali maafikiano kati yao.

Bw Wanyama pia alisema kuwa suala la utunzaji linafaa kushughulikiwa baada ya mtoto kuzaliwa na katika korti ya watoto badala ya mahakama kuu.

Pia ilibainika kortini kwamba Bi Mutaki anamtaka spika amnunulie nyumba ya kifahari na malipo ya Sh200,000 kumwezesha kumtimizia mtoto huyo ambaye bado hajazaliwa mahitaji mbalimbali.

Uhusiano wa kimapenzi kati ya wawili hao ulianza mnamo 2018 na wakatengana mnamo Mei mwaka huu baada ya Bi Mutaki kumweleza Bw Lusaka kuwa alikuwa na mimba yake.

You can share this post!

Ruto akausha mahasla

Sihitaji kuungwa mkono na Uhuru kuingia Ikulu – Raila