Lusaka apuuza uvumi anamezea useneta Bungoma

Lusaka apuuza uvumi anamezea useneta Bungoma

Na BRIAN OJAMAA

SPIKA wa Bunge la Seneti, Kenneth Lusaka amepuuza madai kuwa analenga kuwania kiti cha Useneta wa Kaunti ya Bungoma katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Lusaka alisema kuwa wakazi wa kaunti hiyo wanafamu kiti anacholenga mwaka ujao, akisisitiza kuwa kuwania kiti cha useneta ni kama kurejesha nyuma hadhi yake.

Bw Lusaka anaonekana kama mwanasiasa ambaye ana uwezo wa kung’oa madarakani kwa urahisi uongozi wa sasa wa kaunti hiyo.

Baadhi ya viongozi wa kaunti hiyo wanaoegemea mrengo wa Gavana wa Bungoma Wycliffe Wangamati na naibu wake Charles Ngome wamekuwa wakimrai Bw Lusaka awanie kiti cha useneta.

Ingawa Seneta wa Bungoma, Bw Moses Wetang’ula ametangaza azma yake ya kuwania kiti cha urais, bado haifahamiki iwapo atatetea kiti chake 2022.

Bw Lusaka alikuwa akizungumza katika eneobunge la Tongaren wakati wa mazishi ya Mama Gertrude Naliaka, mamaye Waziri Msaidizi wa Fedha, Eric Wafukho.

“Kwa sasa mimi ni Spika wa Bunge la Seneti. Inawezekanaje niwanie useneta kisha tena niwe nikimwomba spika nafasi ya kuongea? Hiyo ni kama kujirejesha nyuma na wacha niweke bayana kwamba sitawania kiti cha useneta. Wakazi wa Bungoma wanajua kile ninachotaka,” akasema Bw Lusaka.

Prof Ngome wiki jana alinukuliwa akimrai Bw Lusaka awanie kiti cha useneta wa Bungoma. Baada ya mahakama kuharamisha ripoti ya BBI mnamo Alhamisi sasa itambidi Bw Lusaka kurejelea siasa za Bungoma.

Mrengo wa Gavana Wangamati ulitarajia kuwa kupitishwa kwa BBI kungeongeza nyadhifa za juu serikalini na Bw Lusaka angeteuliwa katika moja ya hizo.

  • Tags

You can share this post!

BBI: Uhuru, Raila sasa kusuka mbinu mpya ya mageuzi

Wadau walia sheria za Covid zawafinya