Habari

Lusaka atia muhuri kubanduliwa kwa Murkomen

May 12th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

SASA ni rasmi kwamba Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen na mwenzake wa Nakuru Susan Kihika wamepokonywa nyadhifa za kiongozi wa wengi na kiranja wa wengi, mtawalia.

Hii ni baada ya Spika wa Seneti Kenneth Lusaka kukubaliana na mabadiliko yaliyofanywa katika mkutano wa maseneta wa Jubilee uliofanyika katika Ikulu ya Nairobi Jumatatu.

Mkutano huo uliongozwa na kiongozi wa chama hicho Rais Uhuru Kenyatta.

“Nimeridhishwa na mabadiliko yaliyofanywa katika mkutano huo kwa sababu yanafungamana na sheria za seneti nambari 19. Na yanaafiki hitaji la sheria nambari 19 (5) ya uamuzi uliofikiwa na wengi,” akasema.

Bw Lusaka ameeleza kuwa amepokea kumbukumbu za mkutano huo na orodha ya maseneta 20 waliohudhuria na “kutekeleza mabadiliko katika Uongozi wa Jubilee katika Seneti.”

“Pia nimepokea sahihi za maseneta ambao walihudhuria mkutano wa Mei 11, 2020, katika Ikulu ya Nairobi, hati ya muafaka wa muungano wa baada ya uchaguzi kati ya Jubilee na Kanu na cheti kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Kisiasa cha Mei 8, 2020,” akaongeza.

Kulingana na Lusaka, mrengo wa wengi umeteleza mabadiliko na Seneti sasa inawatambua Seneta wa Pokot Magharibi Samuel Poghisio (Kanu) kama Kiongozi wa Wengi, Irungu Kang’ata kama Kiranja wa Wengi na Seneta Maalum Farhiya Ali kama Naibu Kiranja wa Wengi.