Lusaka awarai wanasiasa Waluhya wasibuni vyama vingine

Lusaka awarai wanasiasa Waluhya wasibuni vyama vingine

Na BRIAN OJAMAA

SPIKA wa Bunge la Seneti Ken Lusaka ametoa wito kwa wanasiasa wa jamii ya Mulembe wakome kubuni vyama vingine vidogo na badala yake wakumbatie au kuunganisha vyama vilivyoko kuelekea uchaguzi wa 2022.

Bw Lusaka alisema vyama vinavyowakilisha maslahi ya wakazi wa eneo hilo tayari vipo na vinafaa viimarishwe zaidi badala ya vingine vidogo kubuniwa.

Alikisia kuwa huenda wanasiasa wanabuni vyama vidogo kwa kuhofia kulemewa wakati wa mchujo wa vyama vikubwa mwaka 2022.

“Tayari tuna vyama ambavyo vina mizizi na vinamilikiwa na wanasiasa kutoka eneo hili. Tunafaa tufanye kazi pamoja badala ya kugawanya jamii yetu kwa kuanzisha vyama vingine zaidi,” akasema Bw Lusaka.

Alikuwa akizungumza nyumbani kwake Mapera alipowaandaliwa wakazi sherehe za Krismasi ambapo alisema taifa linafaa kuwa na vyama viwili au vitatu imara kisha raia wenyewe wajiamulie ni chama kipi cha kujiunga nacho.

Hata hivyo, alivitaka vyama vya kisiasa nchini vihakikishe kuwa vinaendeleza demokrasia hasa wakati wa mchujo ili wanasiasa wawe na imani navyo ndipo wasivibuni vyama vidogo vidogo.

Bw Lusaka ambaye, ametangaza kuwa analenga kuwania kiti cha ugavana wa Bungoma, alisema kuwa atatangaza hivi karibuni chama ambacho atatumia baadaye akisema kwa sasa anayashughulikia masuala muhimu bungeni.

Hivi majuzi Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa alizindua chama cha DAPK ambacho sasa ni nyumbani kwa mbunge wa Kanduyi Wafula Wamunyinyi na mwenzake wa Tongaren Dkt Eseli Simiyu ambao walikuwa kwenye mzozo wa uongozi na nyapara wa Ford Kenya Moses Wetang’ula.

You can share this post!

Maendeleo yameathiri maisha mitaa ya mabanda

Atwoli, Oparanya wakagua Bukhungu matayarisho ya mkutano...

T L