Habari

Lusaka kuandaa kikao kutatua zogo la fedha

August 3rd, 2019 1 min read

Na DENNIS LUBANGA

MGOGORO uliopo kuhusu ugavi wa fedha za kaunti ulichukua mkondo mpya Ijumaa huku Spika wa Seneti, Ken Lusaka akiitisha mkutano kati ya magavana, maseneta na wabunge kutatua mvutano huo.

Spika huyo alisema pana haja ya dharura ya kupanga kikao kati ya pande hizo mbili ili kutatua mzozo huo unaoonekana kuvuka mpaka.

“Kadri ya jinsi tunavyopigia debe kuwepo kwa kikao kati ya pande hizo mbili ili kutatua mzozo kuhusu ugavi sawa wa fedha zinazotengewa serikali za kaunti, ningependa kusema mazungumzo ndiyo suluhisho. Tunataka kila mtu hatimaye aridhishwe na chochote kitakachoafikiwa,” alisema Bw Lusaka.

Alhamisi iliyopita, Baraza la Magavana lilitofautiana vikali huku likikaidi agizo la Rais Uhuru lililotaka wakome kudai nyongeza ya hela kutoka kwa Hazina ya Fedha, na kuashiria kuzidisha juhudi zao za kuitisha nyongeza ya kiasi cha fedha wanachopata kutoka kwa serikali.

Kiasi kikubwa

Wito huo wa kutaka nyongeza ya fedha uliongozwa na mwenyekiti wa Baraza la Magavana Bw Wycliffe Oparanya, ambaye, katika kongamano mjini Nakuru, alisisitiza watashikilia msimamo wao wa kushinikiza serikali kuu kutengea kaunti kiasi kikubwa zaidi cha fedha.

Haya yanajiri baada ya Bunge la Kitaifa kupitisha mswada uliochapishwa tena kuhusu Ugavi wa Fedha ulioonyesha Sh316.6 bilioni kama kiasi cha fedha kikichotengewa serikali za kaunti na kuashiria mchakato mwingine wa majadiliano na Seneti.

Hata hivyo, katika mahojiano Ijumaa na Taifa Leo, Bw Lusaka aliwaomba wawakilishi kutoka mabunge yote kuheshimiana badala ya kurushiana makonde.

“Kama viongozi waliochaguliwa kutoka, tunapaswa kuzungumza na kuelewana,” alisema.