Maabara ya kupima Covid-19 kwenye uwanja wa ndege wa Ethiopia yarahisisha usafiri

Maabara ya kupima Covid-19 kwenye uwanja wa ndege wa Ethiopia yarahisisha usafiri

NA MASHIRIKA

Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bole nchini Ethiopia ambao unahudumia zaidi ya wasafiri milioni 22 kwa mwaka na shirika la ndege la nchi hiyo Ethiopia Airlines ndilo kubwa zaidi barani Afrika.

Lakini wakati huu wa janga la corona, serikali na wizara ya afya nchini humo ilikumbwa na changamoto ya kupima wasafiri virusi vya Covid-19.

Hata hivyo ushirikiano mpya wa serikali ya Ethiopia, BGI Health Ethiopia na kampuni ya BGI Genomics Co., Ltd ya China utawezesha wasafiri kupata huduma ya upimaji kwa haraka na hivyo kuhakikisha safari zao hazijaathiriwa.

BGI Health Ethiopia, ni tawi la kampuni kubwa ya kibayoteki ya China, BGI Genomics.

Shirika la ndege la Ethiopia, linatarajia maabara hiyo, iliyo na teknolojia za hali ya juu, itaongeza kasi inayohitajika kusaidia kupunguza shinikizo kwa utoaji wa huduma za upimaji wa COVID-19 na kwa wakati unaofaa.

“Tunaamini uwezeshaji huu na urahisi utawawezesha abiria wetu kukuza imani yao na kuendelea kusafiri kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole.” anasema Kaimu Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Shirika la ndege la Ethiopia Retta Melaku.

Kulingana na Retta, kituo hicho ni matokeo ya ushirikiano bora kati ya shirika la ndege la Ethiopia na BGI Health Ethiopia kuelekea kuhakikisha usalama wa abiria kulingana na mahitaji yote ya kimataifa.

Maabara hiyo mpya ina uwezo wa kufanya upimaji wa COVID-19 kwa zaidi ya watu 1,000 kwa siku, lakini pia itaongeza uwezo huo hadi vipimo 5,000.

Maabara hiyo pia ndio kubwa zaidi ya hali ya juu na aina yake katika ukanda wa Afrika Mashariki.

BGI Genomics inasema kituo hicho ni sehemu ya ushirikiano unaoendelea kati ya wadau wa China na Afrika hasa kipindi hiki cha kukabili janga la corona na tayari kuna zingine kama hicho nchini Togo, Gabon, Angola na Botswana.

Naibu meneja mkuu wa BGI Health Ethiopia Wanyue Wang, anasema lengo la muda mfupi ni kuhakikisha kuendeleza huduma za usafiri wa ndege kati ya Ethiopia na nchi zingine kwa mazingira salama hata wakati huu wa janga la COVID-19.

“Tunatoa matokeo kwa muda mfupi kama masaa matatu. Sasa, abiria wanaotupitia uwanja huu wakielekea maeneo mengine hawahitaji kutoka nje, wanasubiri matekeo kwenye ukumbi tu” , anasema Wanyue Wang.

Maabara hiyo pia inawezesha abiria wanaoondoka Addis Ababa kufanya upimaji wa haraka wa COVID-19 iwapo watahitaji na kupata matokeo kabla ya kuabiri ndege.

Kituo hicho, kilianzishwa baada ya ombi kutoka kwa shirika la ndege la Ethiopia na hatimaye kuidhinishwa Taasisi ya Afya ya Umma ya Ethiopia (EPHI).

CRI

  • Tags

You can share this post!

Kustawisha afya za watu ndio chanzo cha kujenga taifa...

Mwathi achaguliwa mwenyekiti wa kamati ya usalama bungeni