Habari

Maafa mpaka lini?

October 5th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA, JUSTUS OCHIENG’ na MARY WANGARI

WAKENYA wameendelea kupoteza maisha yao kwenye ajali za barabarani huku maafisa wakuu serikalini na asasi mbalimbali zinazosimamia usalama barabarani zikionekana kulemaa.

Watoto wengi wamebaki mayatima, wanawake wajane na wazazi kupoteza watoto wao kwenye ajali ambazo zinaweza kuepukwa sheria zikitekelezwa na kuzingatiwa kikamilifu. Kwa mara nyingine, usiku wa kuamkia Ijumaa, watu 13 akiwemo mtoto aliyekuwa na umri wa miaka miwili walifariki basi walimosafiria lilipogongana na trela eneo la Awasi, kaunti ya Kisumu.

Ajali hii ilijiri siku mbili baada ya waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiangi kuagiza polisi kushirikiana na Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama kudumisha usalama barabarani.

NTSA iliondolewa barabarani mwaka 2018 ikidaiwa kuzembea katika utekelezaji wa majukumu yake ingawa ilisemekana polisi walihujumu shirika hilo.

Hata baada ya NTSA kuondolewa barabarani, takwimu zinaonyesha idadi ya watu wanaoangamia kwenye ajali barabarani inazidi kuongezeka.

Takwimu za NTSA zinaonyesha kuwa, kufikia Oktoba 1 mwaka huu, watu 2,672 walikuwa wamefariki katika ajali za barabarani ikilinganishwa na watu 2,286 waliokufa kufikia wakati huo mwaka 2018. Hii ni ongezeko la watu 386 wasio na hatia.

Kama kawaida serikali inapotoa taarifa baada ya mikasa ili kujiondolea lawama, Ijumaa, Mkurugenzi wa NTSA Francis Meja na msemaji wa polisi charles Owino waliandaa kikao na wanahabari na kudai ajali nyingi husababishwa na magari ya kibinafsi.

Katika hali iliyoangazia zaidi mahangaiko ya raia wa kawaida, majeruhi katika ajali ya Ijumaa waliokimbizwa hospitali ya Rufaa ya Jaramogi Oginga Odinga (JOOTRH) walijipata katika njia panda walipolazimika kuhudumiwa na wauguzi kufuatia mgomo wa madaktari.

Abiria waliojeruhiwa walirundikana hospitalini huku wakihudumiwa na kundi hilo dogo la maafisa wa afya.

Kulingana na NTSA, idadi ya ajali zilizosababishwa na magari ya kibinafsi iliongezeka kutoka 579 mwaka 2018 hadi 702 mwaka 2019.

Idadi ya ajali zinazohusisha wanabodaboda ambao wanasifika kwa kupuuza sheria pia iliongezeka sawa na wanaotembea kwa miguu. Hata hivyo, ajali nyingi hutokana na utekelezaji duni wa sheria au sheria kupuuzwa kabisa.

Maafisa wa polisi wamehusishwa na ulaji wa hongo ili kuruhusu magari mabovu na yanayokiuka sheria kuhudumu katika barabara za humu nchini.

Idadi yashtua na kutisha

Bw Meja alikiri kwamba idadi ya watu wanaoangamia kwenye ajali barabarani inatisha.

“Idadi ya watu wanaokufa katika barabara zetu iko juu sana na inahitaji mchango wa wadau wote kupunguza ajali hizi,” alisema.

Aliwataka madereva kuwa waangalifu barabarani.

Katika ajali ya Awasi, ilisemekana dereva alikuwa akihepa tingatinga lililobeba miwa alipogongana na trela.

Hii ni hata baada ya matingatinga kupigwa marufuku katika barabara za humu nchini usiku. Kampuni za mabasi zinapaswa kuwa na leseni za kuhudumu usiku ambazo hutolewa baada ya kutimiza masharti makali,. Hata hivyo imebainika baadhi ya kampuni hukiuka kanuni hizi na kuwahonga maafisa wa polisi kusafiri usiku.

Kulingana na msemaji wa polisi Charles Owino, dereva wa lori lililohusika kwenye ajali ya Awasi alikuwa akiliendesha kwa mwendo wa kasi akiwasha mataa. Madereva wa magari hayo mawili ni miongoni mwa watu 13 waliokufa. Ajali ya Awasi iliyohusisha basi la kampuni ya Eldoret Express iliyokuwa ikitoka Rarieda kueleka Nairobi ilijiri siku sita baada ya mwanamke kutumbukia baharini akivuka feri mjini Mombasa.