Habari

MAAFA YA MVUA: Watu tisa waangamia

March 16th, 2018 2 min read

Na WAANDISHI WETU

WATU tisa walifariki katika maeneo mbalimbali ya nchi kutokana na mvua kubwa inayoendelea kunyesha, ambayo pia imesababisha uharibifu mkubwa.

Maafa makubwa yalishuhudiwa katika kaunti ya Kitui ambako watu saba waliaga dunia, baada ya kusombwa na maji, wanne wakiwa watu waliokuwa wanabeba makaa.

Wanne hao waliangamia ndani ya Mto Enziu, Mwingi Mashariki, baada ya lori walimokuwa kuzamishwa na mafuriko. Wanne hao walikuwa wakisafirisha makaa kutoka Yatwa, tarafa ya Nuu, kupeleka Nairobi wakati wa mkasa huo.

Kulingana na aliyeshuhudia kisa hicho, lori hilo lilikwama katikati mwa mto, na waliangamia walipokuwa wakijaribu kulikwamua.

“Waliruka na kujishikilia juu ya lori lakini hawakuwa na bahati kwa sababu lori hilo lilibingirishwa na mafuriko.

Jumanne, watu wawili, mama na mtoto wa miaka saba waliaga dunia walipokuwa wakijaribu kuvuka mto Ikinye, Mwingi.

Wiki iliyopita, mwanamume alisombwa na mafuriko mto Tyaa. Katika eneo la Isiolo, mwanamume wa miaka 30 alisombwa na mafuriko.

Kulingana na Naibu Kamishna wa Kaunti ya Isiolo Otieno Okich, mwanamume huyo Bashir Khallif, alikuwa akivuka mtaro eneo la Soko Mjinga alipoanguka na kusombwa na mafuriko.

Jijini Nairobi, mtu mmoja alisemekana kusombwa Nairobi River, uliojaa hadi pomoni, masaa ya asubuhi wakati wa mvua kubwa.

Wakati huo, Mamlaka ya Uchukuzi na Usalama iliwatahadharisha wananchi na watumiaji wa barabara kuwa makini sana kwa sababu ya mvua.

Mto Nairobi ulipovunja kingo, watu katika eneo hilo walilazimika kutumia njia hatari ya kuvuka barabara, ambapo walionekana kujishikilia kwenye vyuma vinavyokinga Nairobi River kuvuka, au kuvushwa kwa mikokoteni au bodaboda.

Barabara za Moi Avenue, Tom Mboya, Race Course, Ronald Ngala, Haile Selassie Avenue, Temple Road, Kimathi, Uhuru Highway na Kenyatta Avenue katikati mwa jiji la Nairobi zilijaa maji.

Nje ya jiji, hali ilikuwa kama hiyo kwenye barabara za Thika Road, Mombasa Road na Jogoo Road, ambapo maelfu ya watu walitatizika kufika katikati mwa jiji la Nairobi.

Maeneo ya South C, Parklands, Nairobi West, Westlands yalikuwa kati ya maeneo ambayo yaliathiriwa zaidi ambapo nyumba na Shule ya Upili ya Embakasi ziliingia maji.

Katika eneo la Riverside, magari madogo yalionekana kushindwa kuvuka daraja la Nairobi River kwa sababu ya maji mengi eneo hilo.

“Magari yanakwama kwa sababu ya matope na mawe kutokana na ujenzi unaoendelea,” alisema mfanyibiashara mmoja eneo hilo.

Katika eneo hilo, mabomba kadhaa ambayo yamepasuka, mita chache kutoka Nairobi River yalichangia zaidi mafuriko yaliyoshuhudiwa eneo hilo.

“Maji yote ya Nairobi yanakutania hapa kwa sababu barabara ya Racecourse imeinama,” alisema Bw Boniface Njiru, mfanyakazi eneo hilo.