Habari

Maafa zaidi

November 25th, 2019 2 min read

Na WAANDISHI WETU

WAOKOAJI Jumapili waliendelea kusaka miili ya watu 22 wasiojulikana waliko, baada ya maporomoko ya ardhi yaliyoua watu 46 Jumamosi.

Serikali ilisema shughuli hiyo inaendelezwa katika vijiji vya Parua, Nyarkulian na Mwino.

Waziri wa Afya wa kaunti ya Pokot Magharibi, Bw Geofferey Lipale, alisema watu 14 waliojeruhiwa wanatibiwa hospitalini, wawili wakiwa katika hali mahututi.

Zaidi ya watu 200 walioathiriwa na maporomoko hayo wapo kambini katika shule ya msingi ya Nyarkulian, wakihitaji malazi na chakula.

Serikali jana ilipeleka msaada wa chakula kilichosafirishwa kwa ndege lakini hakijawafikia waathiriwa kutokana na hali mbali ya hewa.

Mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika sehemu mbalimbali ya nchi imesababisha hasara kubwa huku watu wengi wakiachwa bila makao na wengine kupoteza maisha.

Katika Kaunti ya Trans-Nzoia mtu mmoja aliuawa na zaidi ya watu 300 kuachwa bila makao huku mvua kubwa ikiendelea kunyesha na kusababisha mafuriko katika eneo la Kaskazini la Bonde la Ufa.

Aliyefariki alikuwa dereva wa bodaboda na alisombwa na mafuriko makubwa katika eneo la Mtiume yaliyosababishwa na mvua kubwa ambayo imevuruga shughuli za kuvuna mahindi katika kaunti hiyo.

Mwendazake, Enos Sasita, 36 alisombwa na mafuriko alipokuwa anajaribu kuvuka daraja la Exodus akielekea eneo la Stabicha.

Shahidi mmoja alisema dereva huyo alikuwa anajaribu kuvuka daraja la Exodus aliposombwa na maji, tukio lilitendeka mwendo wa saa moja jioni.

Kamanda wa polisi katika Kaunti hiyo Bw Ayub Ali alithibitisha tukio hilo na akatoa ushauri kwa watu wote wanaotumia daraja hilo kuwa waangalifu sana.

Waziri wa ugatuzi, Eugene Wamalwa aliwaomba watu wanaoishi katika maeneo yanayokabiliwa na mafuriko katika kaunti hiyo kuhamia katika maeneo salama.

Bw Eugene alitembelea eneo la Namanjalala ambapo watu zaidi ya 300 walibaki bila makao kutokana na mafuriko na kuonya kuwa mvua inayoendelea kunyesha ina hatari kubwa kwa watu wanaoishi karibu na Mto Sabwani.

Kwingine, familia zilizoachwa bila makao baada ya mvua hiyo kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi wameelezea hofu ya kuzuka kwa magonjwa yanayotokana na maji machafu.

Familia hizo zilizo katika kaunti za Pokot Magharibi, Turkana, Baringo na Elgeyo Marakwet jana zilisema hazikuweza kupata huduma za matibabu katika vituo vya afya vilivyokaribu nao baada ya barabara kadhaa kuharibiwa na mvua kubwa.

Mmoja wa wahanga wa mkasa wa maporomoko abebwe kuvuka tope eneo la Serbit, West Pokot. Picha/ Jared Nyataya. i

Katibu Mkuu katika Wizara ya kawi, Simon Kachapin aliwaongoza maafisa wakuu wa serikali na mashirika ya kusaidia binadamu kusambaza chakula na bidhaa zingine muhimu kwa familia zilizokumbwa na maporomoko ya ardhi katika Kaunti ya Pokot Magharibi siku ya Ijumaa kutokana mvua kubwa.

“Familia hizi zinafaa kuhamishwa haraka iwezekanavyo kwa maeneo salama ili kuzuia mlipuko wa magonjwa ya kuambukiza kutokana na hali duni ya usafi,” akasema Bw Kachapin, gavana wa zamani wa Pokot Magharibi.

Maporomoko

Katika kaunti ya Elgeyo Marakwet zaidi ya watu 5,000 katika vijiji vitatu watahamishwa kutokana na maporomoko ya ardhi yanayosababishwa na mvua kubwa.

Familia hizi kutoka vijiji vya Kittony, Embobut na Kakisoo katika kata ndogo ya Marakwet Mashariki zimeshauriwa kuhamia katika maeneo salama ili kuepuka majanga yanayoletwa na maporomoko.

Mashirika tofauti jana yalisema yanakabiliwa na changamoto kufikisha chakula kwa wananchi waliobaki bila makao na wanakumbwa na njaa kutokana na barabara mbovu.

Katika eneo la Kibuline, Tigania Magharibi,familia nyingi zimeachwa bila makao. Sehemu ya mji wa Maua ulisombwa na mafuriko baada ya mto Mboone kufurika.

“Tumepoteza stakabadhi zetu muhimu na pia vitabu vya watoto vilisombwa na mafuriko. Mafuriko haya yamesababishwa na watu walioziba njia zinazopeleka maji katika shamba zetu,” Bi Zaberina Gatitu alisema.

Katika kata ndogo za Ndhiwa na Rachuonyo Kusini nyumba zilisombwa na mafuriko huku tatu zikiachwa bila makao na mali nyingi kuharibiwa.

Kamishna wa kaunti ya Homa Bay Harman Shambi alisema waathiriwa wamehamia kwa jamaa zao na kuwaomba watu katika sehemu zinazokumbwa na mfuriko kuhamia maeneo salama.

Ripoti za OSCAR KAKAI, GERALD BWISA, BARNABAS BII, DAVID MUCHUI na GEORGE ODIWUOR