Habari Mseto

Maafisa 117 watumwa kwa ofisi za ubalozi ugenini

May 28th, 2018 2 min read

Na BENSON MATHEKA

WIZARA ya Mashauri ya Kigeni, imewatuma maafisa 117 kutoka makao yake makuu jijini Nairobi, kuhudumu katika ofisi za kibalozi katika mataifa ya ng’ambo.

Hii ndiyo mara ya kwanza wizara hiyo kuwatuma maafisa wengi kutoka makao makuu hadi nje ya nchi kwa wakati mmoja.

Inajiri pia wakati ambao serikali inapanga kufungua ofisi mpya za kibalozi katika mataifa kadhaa ulimwenguni na hasa Afrika.

Waziri wa Mashauri ya kigeni Balozi Monica Juma aliwaagiza maafisa hao kuripoti katika vituo vyao vipya Juni 15.

Kwenye barua aliyoandika Mei 23, Bi Juma anasema kwamba maafisa hao watahudumu kwa miaka minne katika vituo hivyo na kuwakumbusha kuwa kazi katika ofisi za kibalozi huwa ya muda.

“Mnakumbushwa kuwa huduma katika ofisi za kibalozi ng’ambo huwa ni ya muda na ina majukumu yanayopaswa kufanywa kwa kipindi fulani.

Kipindi cha kuhudumu kinaweza kubadilishwa kwa kuzingatia hali ya kazi na kanuni za huduma kama vile utendakazi, mahitaji ya kuendesha ofisi ya kibalozi au katika makao makuu, umri wa kustaafu ukiwa ng’ambo au ukosefu wa nidhamu,” alisema Bi Juma kwenye barua yake.

Hatua ya wizara inajiri wakati ambao serikali inang’ang’ana kupigana na kashfa za ufisadi katika asasi za umma.

Mnamo 2016, ripoti ya Mhasibu Mkuu wa serikali Edward Ouko ilifichua kuwa afisi za kibalozi hazikuweza kuthibitisha mapato ya viza na paspoti ya thamani ya Sh1.5 bilioni.

Bi Juma alisema kwamba maafisa hao watapatiwa mafunzo na kukaguliwa na chuo cha mafunzo kuhusu huduma katika ofisi za kibalozi (FSA) kabla ya kuanza kazi katika vituo vipya.

“Maafisa wote waliotambuliwa na kuteuliwa kwenda kuhudumu watapatiwa mafunzo na chuo cha mafunzo kuhusu huduma za kazi za kibalozi na baada ya hapo watakaguliwa na kuidhinishwa,” alisema Bi Juma kwenye barua yake.

Kwenye barua yake, Bi Juma anasema “ilikubaliwa maafisa hao watumwe katika vituo hivyo” lakini hatoi maelezo zaidi. Hatima ya maafisa wanaohudumu katika ofisi zilizoathiriwa haijulikani.

Maafisa hao watatekeleza majukumu mbali mbali katika ofisi za kibalozi na mashirika ya Umoja wa Mataifa kama Unesco.

Kulingana na Bi Juma, watakuwa wakihudumu chini ya mabalozi wa Kenya katika nchi walizotumwa kuhudumu.

Alisema kwamba wataendelea kutekeleza majukumu yao ya sasa hadi tarehe ambayo wataruhusiwa kuondoka rasmi kwenda katika vituo vyao vipya.