Habari Mseto

Maafisa 160 wa magereza kusoma kwa muda wa miezi 13 Ruiru katika kiwango cha Cadet

December 12th, 2020 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

MAAFISA wa magereza wapatao 160 wataanza mafunzo rasmi kwa muda wa miezi 13 Ruiru katika kiwango cha Cadet.

Waziri wa Usalama na Maswala ya Ndani, Dkt Fred Mating’i alisema mpango huo ni wa mwanzo kuzinduliwa na serikali magerezani na ukiwa umejumuisha jinsia zote mbili.

Alisema baadhi ya masomo watakayozingatia ni sheria, uongozi, usimamizi na maswala mengine muhimu ya kushughulika na wananchi.

“Nimefurahishwa na maafisa na hasa nyinyi ambao mmejitolea kuhudumia wananchi kwa kujihami na ujuzi zaidi. Serikali iko tayari wakati wowote kuwaunga mkono ili kuafikia malengo yenu,” alisema Dkt Matiang’i.

Aliahidi atafanya juhudi kuona ya kwamba ajenda muhimu za serikali zinazoelezwa na Rais Uhuru Kenyatta zinatekelezwa kikamilifu.

“Tunataka kuona magereza yetu yanageuzwa kuwa pahala pa kurekebisha tabia wala sio kutesa wafungwa. Tunataka kuona maafisa wa magereza wakiwarekebisha wafungwa wala sio kuwadhulumu,” alisema waziri huyo.

Aliyasema hayo mnamo Alhamisi katika chuo cha magereza cha Ruiru alipohudhuria kuwakaribisha maafisa wapya wa cadet walioanza mafunzo yao.

Katibu katika wizara hiyo Karanja Kibicho alisema maafisa hao waliojiunga kuwa katika kiwango cha Cadet wanastahili kuonyesha nidhamu ya hali ya juu ili wajitambulishe vilivyo kwa umma.

“Nyinyi kama maafisa waliotambulika ni sharti muonyeshe nidhamu na mwelekeo mwema kwa umma. Kwa hivyo nawatakia heri njema kwa masomo yenu,” alisema Bw Kibicho.

Kamishna mkuu wa magereza Bw Wycliffe Ogallo alisema maafisa hao walioteuliwa ni miongoni mwa wengi waliopita mtihani na mahojiano mazito kabla ya kupewa nafasi hiyo.

“Maafisa hawa wamepitia mahojiano mazito miongoni mwa wengi waliojiwasilisha,” alisema Bw Ogallo.

Alisema mwezi Agosti 2020, maafisa wa magereza wapya wapatao 3,000 walifuzu na wametumwa kote nchini kutumikia serikali.

Mkutano huo ulihudhuriwa na maafisa kadha wa magereza huku kila mmoja akizingatia sheria za kuzuia homa ya Covid-19.