Habari Mseto

Maafisa 3 wa KRA wanaswa na dawa za kulevya

April 29th, 2018 1 min read

Na MWANDISHI WETU

Maafisa watatu wa KRA walikamatwa na kiwango kikubwa cha dawa za kulevya aina ya Mandrax, katika Uwanja wa Ndege wa Eldoret Ijumaa.

Walikamatwa baada ya maafisa wa polisi kudokezewa kuhusiana na dawa hizo zilizokuwa zimefichwa kama vitamini.

Inasemekana uwanja huo hutumiwa sana kupitishia dawa za kulevya nchini.

Afisa wa polisi ambaye hakutaka kutajwa alisema kulikuwa na operesheni kama hiyo katika jumba moja eneo la Kasarani, Nairobi.

Mwanamume anayeaminika kuwa kiongozi katika biashara hiyo alikamatwa katika eneo hilo.

Maafisa wa GSU walitolewa kwenda katika Uwanja wa Ndege wa Eldoret baada ya mgogoro kuzuka kati ya maafisa wa KRA na maafisa wa polisi uwanjani humo.

Mgogoro huo ulitokana na operesheni iliyoweka wazi ushirika kati ya maafisa hao na wahalifu.

Maafisa hao walisema operesheni hiyo ilitokana na malalamishi kuhusiana na kuzembea kwa maafisa waliokuwa wakishirikiana na wahalifu hao na kutia maelfu ya wananchi katika hatari kubwa.